Femata kuandamana nchi nzima kumpongeza JPM

11Feb 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Femata kuandamana nchi nzima kumpongeza JPM

SHIRIKISHO la Vyama vya Wachimbaji Madini (FEMATA), linatarajia kufanya maandamano ya amani nchi nzima ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuondoa baadhi ya kodi zilizokuwa kero kwa wachimbaji.

rais john magufuli, picha mtandao

Hatua hiyo, inatokana na serikali kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 2 wa mwaka 2019 kwa hati ya dharura bungeni ili kuzifanyia sheria zinazokwamisha sekta ya madini.

Muswada huo ambao ulipitishwa juzi na Bunge, akiwasilisha maelezo ya muswada huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adelardus Kilangi, alisema katika Sheria ya Kodi ya Mapato sura namba 332, kifungu cha 83B umeondoa kodi ya zuio ya asilimia 5 kwa wachimbaji wadogo ili kuhamasisha wachimbaji hao kuuza madini yao kwenye masoko ya madini.

Aidha, alisema Sheria ya Madini sura ya 123 katika kifungu cha 27C imefanyiwa marekebisho ili kuweka ulazima wa ununuzi na uuzaji wa madini kufanywa katika masoko ya madini isipokuwa kwa wamiliki wa leseni kubwa na kati.

Pia, alisema katika Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) sura ya 148, imefanyiwa marekebisho kwa kuongeza kifungu cha 55B ili kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye madini ya metali na vito yanayouzwa na wachimbaji hao kwenye masoko.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi katika viwanja vya Bunge baada ya kupitishwa muswada huo, Rais wa FEMATA, John Bina, alisema maandamano hayo yatafanyika Februari 16, mwaka huu nchi nzima, ambapo wachimbaji wataandamana kwenye mikoa yao.

“Dhamira ya maandamano haya ni kumuonyesha Rais Magufuli upendo na kufurahishwa na kitendo alichokifanya kwa wachimbaji,” alisema.

Alisema Rais amedhihirisha kuwajali wachimbaji wadogo na anataka sekta ya madini ikue ili siku moja atokee mchimbaji mkubwa wa madini wa kitanzania miongoni mwao.

“Maandamano haya yataanzia katika maeneo yao wanayochimba kwenda kwa wakuu wa mikoa kwa kadri itakavyopangwa katika mkoa husika,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), Salma Kundi, alisema pamoja na pongezi hizo wanamwahidi Rais kuwa watashirikiana na serikali ili kudhibiti utoroshwaji wa madini.

"Tunamwahidi tutafanya kazi kwa kufuata sheria na kulipa kodi na tutajitahidi kusaidiana na serikali ili kudhibiti utoroshaji na tutakuwa bega kwa bega kusimamia madini,” alisema.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la FEMATA, Lista Festo, alisema: “Rais ameonyesha kwa dhati mapenzi yake kwa Watanzania waliopo katika sekta ya madini, baada ya siku 17 muswada wenye nia ya kuongeza mapato na kusaidia wachimbaji umeletwa bungeni, tunamshukuru sana,” alisema Festo.

Habari Kubwa