Fursa ya soko la tumbaku yapatikana

07Sep 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Fursa ya soko la tumbaku yapatikana

BUNGE limeelezwa kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020/21, Tanzania imepata masoko mapya ya kuuza tumbaku kwa majaribio katika nchi tatu.

Katika kutekeleza hilo, serikali inatarajia kukutana na uongozi wa kampuni ya TLTC mwishoni mwa mwezi huu ili kuirejesha.

Wizara ya Kilimo ilitoa majibu hayo bungeni jana ilipokuwa ikijibu swali la Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret Sitta.
Katika swali lake, mbunge huyo alihoji serikali ina mpango gani wa kuwezesha kampuni za wazawa ili yawalipe wakulima mara wanaponunua tumbaku yao.

“Suala la kupata wanunuzi zaidi wa kununua tumbaku ni la muda mrefu; Je, kuna mafanikio yaliyopatikana?” Alihoji.

Katika majibu ya wizara hiyo, ilisema serikali inaendelea na jitihada za kutafuta soko la tumbaku katika nchi mbalimbali hasa nchi za Uarabuni, Afrika na Ulaya.

Ilitaja masoko hayo mapya ya majaribio kuwa ni katika nchi ya Romania (tani 200), Poland (tani 100) na Uturuki (tani 50).
Aidha, ilisema sampuli za tumbaku zimetumwa nchini China na Korea Kusini kwa ajili ya masoko hayo.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, kwa muda mrefu biashara ya tumbaku imekuwa ikiendeshwa bila kampuni za kizawa kushiriki katika biashara ya tumbaku na kampuni za nje pekee ndizo zilikuwa zinashiriki katika biashara ya tumbaku.

Ilisema wakati wa ununuzi wa tumbaku kupitia kampuni za nje ununuzi wa tumbaku umeshuka hadi kufikia tani 42,000 za mkataba na baada ya kampuni za wazawa kuingia katika ununuzi uzalishaji umeongeza kufikia tani 68,571 za tumbaku kupitia kilimo cha mkataba.

Aidha, katika masoko ya tumbaku msimu wa kilimo 2020/21 jumla ya kampuni tisa zinanunua tumbaku ya wakulima zikiwamo kampuni saba za wazawa.

Hata hivyo, ilisema kampuni hizo zimekuwa zikikabiliwa na kero ya kupata mitaji ya kutosha hali inayosababisha kuchelewa kuwalipa baadhi ya wakulima.

“Katika kutatua changamoto hiyo, Mei, 2021 Wizara ya Kilimo ilikutanisha kampuni za wazawa na taasisi za fedha kwa lengo la kukubaliana masharti nafuu yatakayowezesha kampuni hizo kupata mikopo kwa riba nafuu,” ilisema.

Ilieleza kuwa mafanikio ya majadiliano hayo yameanza kupatikana ambapo Benki ya CRDB imeridhia kuzikopesha kampuni mbili za Mo Green International na Magefa Growers Limited.

Ilisema serikali inaendelea kushirikiana na kampuni za ununuzi wa tumbaku na taasisi za fedha katika kutatua kero hiyo kwa lengo la upatikanaji wa soko la uhakika la tumbaku na malipo ya wakulima kwa wakati.

 Wizara ilisema ni muhimu kama nchi kuendelea kulea kampuni za wazawa ili ziwe na uwezo wa kununua tumbaku kama kampuni za kigeni na kuziunganisha kampuni za wazawa taasisi za kifedha ili kupata huduma za kifedha ikiwamo kupata Letter of Credit (L.C).