Galawa ang’aka vijana wanawake kutopewa mikopo

20Dec 2016
Nebart Msokwa
MBOZI
Nipashe
Galawa ang’aka vijana wanawake kutopewa mikopo

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa, ameujia juu uongozi wa Halmashauri ya Mbozi kwa kushindwa kutoa mikopo kwa vijana na wanawake ya asilimia 10 ya mapato yake, badala yake fedha zimeelekezwa kwenye matumizi mengine.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa.

Hatua hiyo aliichukua jana kwenye mkutano wa hadhara baada ya malalamiko ya mkazi wa Vwawa, Said Adamu, aliyetaka kujua ahadi ya serikali ya kukopesha mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana na wanawake, kutoiona.

Akijibu, Ofisa Maendeleo ya jamii, Msolini Dakawa, alisema mikopo imeendelea kutolewa licha ya kuwa ni kidogo na hadi sasa zaidi ya Sh. milioni 39 zimekopeshwa katika nusu ya mwaka huu wa fedha na inaendelea kadri fedha zinavyopatikana.

Akifafanua, alisema fedha hizo zimetolewa kwa vikundi 20 vya wanawake na 10 vya vijana ambapo imeidhinishwa wiki iliyopita na kamati ya mikopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Edna Mwaigomole, akitoa ufafanuzi, alisema halmashauri yake imeshindwa kutekeleza agizo hilo kutokana na kutingwa na kazi za utengenezaji wa madawati katika msimu uliopita na kuwa fedha hizo zitatolewa katika kipindi hiki kinachoendelea.

Alisema halmashauri katika nusu ya mwaka wa fedha uliopita imekusanya zaidi ya Sh. 1.5 bilioni ambapo ilistahili kuwa iwe imetoa mikopo kwa makundi ya vijana na wanawake zaidi ya Sh. milioni 150, lakini haikufanikiwa kutokana na changamoto ya mwingiliano wa majukumu.

Hata hivyo, alisema sababu hizo hazikumridhisha mkuu huyo na kuwaambia kushindwa kutoa fedha hizo kwa makundi husika ni sawa na kutengeneza bomu kwa serikali ambalo litaleta tatizo baadaye na ni kuwadhulumu wanyonge haki yao ya msingi.

"Serikali ilipoweka utaratibu huo ilijua kuwa halmashauri zina majukumu mengi, lakini mnashindwa kufanikisha haya kutokana na uzembe wenu wa kushindwa kukusanya mapato ya ndani, lakini kama mngekuwa mnaumiza vichwa kutafuta mapato haya yasingewasumbua,” alisema.

Aliiagiza halmashauri kukamilisha kutoa mikopo iliyosalia ifikapo mwezi Februari mwakani na taarifa aipate mapema ofisini kwake.

Aliwataka wataalamu wote wa idara ya maendeleo ya jamii kuhamia katika vijiji ambako ndiko kwenye watu ili wakawaelimishe namna ya kutumia mikopo hiyo ili iweze kutumika kama mbegu.

Habari Kubwa