Geita washauriwa kurasimisha biashara

21Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Geita
Nipashe
Geita washauriwa kurasimisha biashara

MKUU wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali (mstaafu), Ezekiel Kyuga, amewashauri wafanyabiashara mkoani humu kurasimisha biashara zao kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) zao ili zitambulike kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa semina elekezi juu ya majukumu ya Brela Meja Jenerali Kyuga aliwaeleza wafanyabiashara kuwa kurasimisha biashara kuna faida zake.

Alizitaja faida hizo kuwa ni biashara au kampuni kutambulika, kulindwa na kusaidiwa kwa mujibu wa sheria, kulipa kodi ili kujenga uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi, kuondoa dhana duni ya kufanya shughuli kwa mazoea na kutengeneza mazingira bora ya biashara nchini kwa faida ya kila mwananchi na hasa wafanyabiashara wenyewe.

Alisema sekta ya biashara ina nafasi kubwa katika utekelezaji wa hazima ya serikali ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

“Ili kutengeneza mazingira bora ya biashara nchini, ni muhimu kurasimisha kila biashara zitambulike kwa mujibu wa sheria,” alisema Meja Jenerali Kyuga.

Mkuu wa Mkoa alishauri wafanyabiashara watumie fursa ya kuwapo kwa maofisa wa Brela mkoani kurasimisha biashara zao.

“Brela wametuthamini. Wametufuata huku tuliko. Tutumie nafasi hii vizuri ili turasimishe shughuli zetu kwa urahisi,” alisema.

Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi, alisema wakala huyo amefanya maboresho mengi katika huduma za usajili na kuongeza kwamba lengo la kuwapo mkoani kwa wiki moja, ni kutoa elimu ya urasimishaji biashara, kuwapa fursa wananchi kusajili majina ya biashara na kampuni na kuwaomba wakazi wa Geita kurasimisha biashara zao katika kipindi hiki.

Kanyusi alieleza kuwa usajili wa majina ya biashara unafanywa kwenye mtandao, hivyo mfanyabiashara hana sababu ya kusafiri hadi Dar es Salaam na kuongeza kuwa Brela inapigana ili huduma zote za usajili wa majina ya biashara, kampuni, alama za biashara zipatikane kwa njia ya mtandao ifikapo Machi, mwakani.

Alieleza kwamba biashara inakuwa rasmi inapokuwa na cheti cha Brela, nakala ya namba ya mlipa kodi(TIN) na Leseni ya Biashara na kueleza huo ndiyo msingi wa elimu inayotolewa na wakala juu ya urasimishaji biashara.

Katibu wa TCCIA mkoani Geita, Mariam Mkaka, aliishukuru Brela kwa uamuzi wake wa kufungua ofisi za kanda na kuahidi kwamba wafanyabiashara watarasimisha biashara zao.

Brela inaendelea kutoa semina elekezi na usajili wa majina ya biashara na kampuni kwa Kanda ya Ziwa ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kutoa elimu kwa kanda zote nchini.

Habari Kubwa