GePG ilivyoongeza makusanyo serikalini

18Sep 2020
Ibrahim Joseph
Dodoma
Nipashe
GePG ilivyoongeza makusanyo serikalini

IMEELEZWA kuwa kupitia mfumo wa kielektroniki (GePG), serikali imeongeza makusanyo ya kila mwezi na kupunguza gharama za uendeshaji.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, kupitia mfumo huo makusanyo ya mwezi yameongezeka kutoka Sh. bilioni 668 mwaka 2015/2016 hadi kufikia Sh. trilioni 2.6 mwezi juni, 2020.

Akiwasilisha juzi matokeo ya utafiti wa mfumo huo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Joel Mtebe, alisema tathmini iliyofanywa kwenye mfumo huo ni katika ukusanyaji wa kodi, maduhuli, tozo na huduma mbalimbali.

Alisema mfumo huo umeongeza uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma na kupata taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo.

“Kwa mfano Mamlaka ya Maji Kasuru walikuwa wanatumia kati ya Sh. milioni 1 hadi 1.5 kwa mwezi kusambaza ankra za maji kwa kutumia pikipiki, lakini imepungua kwa kiasi kikubwa ambapo kwa sasa wateja wanapata kupitia mfumo huu,” alisema Prof. Mtebe.

Aidha, alisema Shirika la Umeme nchini(Tanesco), wameokoa Sh. bilioni 38 ambazo zilikuwa zinatumika kwa mwaka kuwalipa mawakala wa kuuza umeme.

“Pia Wakala wa Misitu (TFS) makusanyo yameongezeka kutoka Sh. bilioni 95 kwa mwaka hadi Sh. bilioni 115, Wakala wa Vipimo (WMA) mapato yameongezeka kutoka Sh. bilioni moja kwa mwezi hadi Sh. bilioni 2.5,” alisema.

Alisema kupitia mfumo huo wananchi wanafanya malipo mahali popote bila kupoteza muda wa kwenda maofisini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), William Erio, alisema mfumo huo umeongeza mapato ya shirika kutoka Sh. bilioni 694 mwaka 2018/19 hadi Sh. trilioni 1.1, Juni 2020.

Erio alisema mfumo huo umesaidia kuondoa malipo hewa yaliyokuwa yakifanyika kwa njia ya kuandika hundi bandia zilizokuwa zinalisababishia hasara shirika.

Kadhalika, alisema mfumo huo umefanikisha kuongeza thamani ya shirika kutoka Sh. trilioni 3.4 hadi kufikia Sh. trilioni 4.4 Juni 2020 na umepunguza gharama za uendeshaji kutoka akaunti 78 na kubaki tatu tu pamoja na kuweka uwazi kwa wateja wao na kupunguza miamala.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, aliwashukuru watafiti hao kwa kuandaa na kufanikisha utafiti huo ambao unaonyesha kuwa serikali imebuni mfumo sahihi wa ukusanyaji mapato.

James alisema serikali imebuni mifumo minne ya kielektroniki ambayo imetengenezwa na kusimamiwa na wizara hiyo hivyo ni salama kwa sababu inaendeshwa bila kuingiliwa na mtu wa nje.

Habari Kubwa