H’shauri zatakiwa kuanzisha magulio kulinda wakulima

06Aug 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
H’shauri zatakiwa kuanzisha magulio kulinda wakulima

KAIMU Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA), mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Malanga, amezishauri halmashauri za wilaya katika mikoa hiyo, kuanzisha magulio ya pamoja mahususi kwa ajili ya kuuza mazao kwa kutumia mizani ambayo imekidhi vigezo lengo likiwa ni kuondokana na matumizi ya ndoo na ..

ndonya ambazo zinamuibia mkulima.

Malanga alitoa wito huo jana wakati akizungumza na Nipashe kuhusu utoaji elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya vipimo vilivyothibitishwa na wakala huyo.

Alisema ili kudhibiti wimbi la matumizi ya ndoo na ndonya katika kuuza na kununua mazao ni vyema sasa halmashauri za wilaya katika mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini zikaanzisha magulio ya pamoja ambayo yatakuwa ni kitovu cha uuzaji na ununuzi kwa kuwa na mizani rasmi.

Alisema njia hiyo itamsaidia mkulima kupata faida baada ya kuuza mazao yake kuliko ilivyo sasa wafanyabiashara ndio wananufaika zaidi.

“Maeneo ya vijijini ndiko kuna shida kubwa ya matumizi ya ndoo na ndonya, hawatumii kabisa mizani kuuza mazao yao, na wafanyabiashara wanapenda kweli kwa sababu wanapata faida, nazishauri halmashauri kutenga masoko maalumu ya uuzaji mazao na kuweka mizani ambayo itatumiwa katika uuzaji na ununuzi,” alisema Malanga.

Alisema Wakala wa Vipimo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini utaanza operesheni ya kukagua bucha zote za nyama kuangalia utekelezaji wa agizo la kuhakikisha mizani zote zimepigwa chapa na wakala huyo.

Alisema bucha itakayobainika mizani yake haina chapa, itatozwa faini pamoja na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.

Aliwakumbusha wananchi kutokubali kuuziwa nyama au kitoweo chochote katika bucha bila kupimwa kwenye mizani iliyothibitishwa na wakala wa vipimo na wanapobaini kuwa hawajafuata maagizo hayo watoe taarifa mara moja.

Habari Kubwa