H’shauri zatakiwa kuchangamkia fedha za miradi

14Oct 2021
Faustine Feliciane
Kahama
Nipashe
H’shauri zatakiwa kuchangamkia fedha za miradi

HALMASHAURI za wilaya zinazozunguka mgodi wa Bulyanhulu mjini Kahama zimetakiwa kuandaa miradi yenye manufaa, kwa ajili ya kufadhiliwa na mgodi wa Barrick unaomilikiwa kwa pamoja na serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation Limited.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukurani Manya, wakati wa kikao na uongozi wa kampuni ya Barrick chini ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu, Mark Bristow na waandishi wa habari.

Alisema Kampuni ya Barrick ipo tayari kuwekeza kwenye maeneo yanayozunguka mgodi huo, lakini kwa kufuata sheria na utaratibu walizojiwekea.

"Pamoja na kuandaa miradi hiyo ni lazima nidhamu ya matumizi ya pesa iwepo, hakuna mtu au kampuni inayopenda kutoa pesa zake halafu wasione matunda ya pesa hizo ni lazima hiyo miradi itakayopitishwa isimamiwe kikamilifu na kuhakikisha kila pesa inaenda kufanya kazi iliyokusudiwa," alisema Prof. Manya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Barrick, Bristow, alisema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na jamii inayozunguka migodi yake katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Alisema Barrick imeanza mchakato wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kahama Bulyanhulu, kwa ajili ya kuwezesha huduma za usafiri kwa wananchi.