H’shauri zatakiwa kujenga urafiki wafanyabiashara kulipa kodi

09Jan 2019
Happy Severine
Bariadi
Nipashe
H’shauri zatakiwa kujenga urafiki wafanyabiashara kulipa kodi

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, amezitaka halmashauri zote za mkoa huo, kuacha tabia ya kuwafungia wafanyabiashara maduka yao wanapochelewa kulipia leseni na badala yake waangalie utaratibu rafiki utakaowezesha kulipa fedha hizo kwa wakati.

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, picha mtandao

Agizo hilo alilitoa jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kifurushi cha kitu bomba cha Halotel kinachoendeshwa kwa ubia wa Godtec, uliofanyika mjini Bariadi.

Mtaka alisema haiwezekani halmashauri zikawa zinawafungia wafanyabiashara maduka kwa sababu tu ya kuchelewesha fedha za leseni, badala yao wabuni mbinu rafiki itakayowafanya wafanyabiashara wenyewe kulipa kwa wakati.

Alisema kitendo cha kuwafungia maduka wafanyabiashara hao, kinasababisha kuzaliwa chuki miongoni mwao na serikali yao hivyo ni vema sasa maofisa biashara wakatafuta mbinu mbadala ya kuwafanya na kuwashawishi kulipa bila kufuatiliwa na kwa wakati.

Mtaka alisema Mkoa wa Simiyu umeingia katika historia ya kuwa na huduma bora ya kimtandao wa kifurushi cha kitu bomba cha Halotel ambacho lengo kuu ni kuzalisha ajira kwa Watanzania na kukuza biashara na taaluma za watu kupitia mtandao.

Alisema kuzinduliwa kwa kifurushi cha kitu bomba mkoani Simiyu chenye vifurushi maalumu vya kundi la taaluma na kundi la wateja wote kutachangia kukuza uchumi katika biashara ya mtandao.

Aidha, balozi wa kampeni hiyo, Jacob Steven, aliwasihi Watanzania wote kwa ujumla kununua line za Halotel, ili waweze kujiunga na kifurushi hicho kitakachowasaidia kufanya biashara zao kimtandao.

Habari Kubwa