Hali ya biashara yazidi kuimarika

14May 2022
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Hali ya biashara yazidi kuimarika

WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Omar Said Shaaban, amesema hali ya biashara imeendelea kuimarika kwa kipindi cha mwaka 2021.

WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Omar Said Shaaban.

Amesema katika kipindi hicho , Zanzibar imefanya biashara yenye thamani ya Sh. trilioni 1.12 ikilinganishwa na Sh. bilioni 913.09 kwa mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 23.1.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi jana, alisema biashara hiyo ilikuwa usafirishaji wa bidhaa kwenda nje ya Zanzibar na uagiziaji wa bidhaa kuingia Zanzibar.

Waziri Omar alisema mwaka wa fedha 2021/22 Zanzibar imeagiza bidhaa zenye thamani ya Sh.  bilioni 7.823 kutoka nchi za kusini mwa Afrika, ambayo ni sawa na asilimia 0.8 ya uagiziaji wote.

“Uagiziaji wa bidhaa kwa nchi za SADC kwa mwaka 2021 umeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2020 ambapo bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni 6.15 ziliagizwa,” alisema.

Alisema Afrika Kusini imeongoza kwa kuingiza bidhaa Zanzibar zenye thamani ya Sh. bilioni 6.88 kwa mwaka 2021 kwa bidhaa za nguzo za mbao.

Pia alisema kwa mwaka wa fedha 2021/22 Zanzibar imesafirisha nje bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni 155.62, kiwango hicho cha usafirishaji ni sawa na ongezeko la asilimia 137 ikilinganishwa na usafirishaji wa bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni 65.66 uliofanyika kipindi cha mwaka 2020.

Alisema bidhaa zilizosafirishwa nchi za nje ni pamoja na karafuu, mwani na mazao ya baharini na katika usafirishaji huo, zao la karafuu lilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 115.36 sawa na asilimia 74.1 ya usafirishaji wote.

 “ Ongezeko hilo limechangiwa na kupanda kwa bei ya karafuu na msimu mkubwa wa uzalishaji. Miongoni mwa nchi zilizonunua karafuu ni pamoja na Singapore, India, Denmark na nchi za Falme za Kiarabu (UAE),” alisema.

Habari Kubwa