Halmashauri 20 zategwa fedha mipango miji

15Feb 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Halmashauri 20 zategwa fedha mipango miji

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, amesema Halmashauri 20 zinasuasua katika utekelezaji wa mpango wa upangaji mji licha ya serikali kutoa fedha.

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, picha mtandao

Kufuatia hali hiyo, Mabula amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuzichukulia hatua halmashauri zilizotumia fedha hizo kinyume na masharti waliyopewa.

Mabula alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha miji yote inapangwa vizuri na inakuwa salama kwa makazi ya watu lakini mpango umesuasua kwa halmashauri kutokana na kutokuwa waaminifu.

“Serikali ilitoa fedha zaidi ya Sh.Bilioni 6.2 ya kupanga kwenye halmashauri zetu ambao uliwezesha 24, mpango unasuasua kutokana na halmashauri nyingi kutokuwa waaminifu, tumepeleka fedha kwa Halmashauri 24 lakini ni nne tu ndio zimetekeleza,” alisema.

Mabula alitaja Halmashauri zilizotekeleza kuwa ni Mbeya, Ilemela, Kahama na Bariadi huku zingine zikichukua fedha bila kufanya kazi hiyo.

“Miji mingine imechukua fedha na haijarejesha, katika hili tunaongeza kasi kwenye ufuatilia, nakuomba Waziri Mkuu, kuchukua hatua kwa halmashauri ambazo zimechukua fedha na kutumia fedha kwa kutozingatia masharti waliyopewa wanasababisha kusuasua kupanga miji yetu,” alisema.

Mabula alisema kupitia mpango huo miradi mbalimbali imeanza kutekelezwa ikiwemo upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi ambapo viwanja 132,000 vimepimwa na zaidi ya laki mbili bado hajivapimwa katika jiji hilo.

“Tuna Imani kasi itakuwa nzuri soko, stendi zimejengwa, tunaamini utekelezaji utaendelea kwa matakwa ya mpango ulivyo,” alisema.

Aidha, alisema kudorora kwa uchumi katika miaka ya 1980 na kubadilika kwa dhana ya upangaji uandaaji wa mpango kabambe katika miji mbalimbali ilififia.

“Dhana iliyopendekezwa ni upangaji wa miti kimazingira kwa kuangalia mazingira yake lakini pia kutayarisha mipango kabambe endelevu, kufifia kwa kasi kunatokana na kudorora kwa wataalam wetu katika uandaaji wa mipango kabambe,”alisema.

Alisema serikali haikukaa kimya, ilichukua hatua mbalimbali ya kufanya miji iwe mizuri ikiwa ni pamoja na kuwa na sera ya maendeleo ya makazi ya mwaka 2000, na kupitisha sera ya mipango miji

Awali, Katibu wa Kikosi Kazi cha Taifa cha kuratibu Mpango wa serikali kuhamia Dodoma, Meshack Bandawe, alisema ujenzi wa mji wa serikali kwa awamu ya kwanza umefanyika.

Alisema mpango kabambe umekamilika na mchoro wa awamu ya pili pia umekamilika huku akisema kiasi cha Sh.Bilioni 88 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kujenga barabara za lami zenye urefu wa kilometa 40 katika mji wa serikali.

“Nyumba 1,000 zinatarajiwa kujengwa na Shirika la Nyumba ambapo 200 zitajengwa katika mji wa serikali,”alisema.

Bandawe alisema majengo ambayo yalikuwa yakitumiwa Dar es salaam, baadhi yameshatolewa kwa taasisi za serikali na kuokoa Sh.Bilioni 9.9 ambazo zilikuwa zikitumika kulipa kodi ya pango.

Habari Kubwa