Halmashauri yatangaza kutoa mkopo mil. 150/- kwa vikundi

15Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Monduli
Nipashe
Halmashauri yatangaza kutoa mkopo mil. 150/- kwa vikundi

HALMASHAURI ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, inatarajia kutoa mkopo wa Sh. milioni 150 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Steven Ulaya, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuhusu mafanikio ya kiutendaji katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais John Magufuli katika halmashauri hiyo.

Alisema katika kipindi hicho, halmashauri hiyo imeongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kutoka Sh. bilioni 2.18 kwa mwaka 2015 hadi kufikia Sh. bilioni 2.24.

Alisema ongezeko hilo limeiwezesha halmashauri mwaka uliopita kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ya Sh. milioni 430.4 tofauti na mwaka 2015, ambapo walitoa mikopo
Sh. milioni 63.7 tu.

Mapema akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa miaka mitatu wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Iddy Kimanta, alisema miradi iliyofanikiwa kwa kiasi kikubwa ni sekta ya elimu.

Alisema kwa mwaka 2015 wilaya hiyo ilikuwa inapata Sh. milioni 393 za elimu kutoka Serikali Kuu lakini sasa wanapata Sh. bilioni 3.6.

Alitaja sekta nyingine iliyofanikiwa kuwa ni afya ambayo kwa upande wa vifaa tiba na dawa kwa mwaka 2015, ilipata Sh. milioni 176.28, lakini kufikia mwaka jana fedha ziliongezeka hadi kufikia Sh. milioni 576.52.

Alisema licha ya dawa na vifaa tiba pia wamepokea Sh. milioni 800 kutoka Serikali Kuu, ambazo zimeboresha vituo vya afya vya Mto wa Mbu na Makuyuni kwa kujenga jengo la kutoa huduma za mionzi, jengo la upasuaji, maabara pamoja na jengo la huduma za mama na mtoto.

"Ongezeko la upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na dawa umesaidia wananchi kupata huduma bora za afya, na kupunguza vifo haswa vya wanawake wajawazito wakati wa kujifungua, kutoka 161 kwa mwaka 2015 hadi kufikia vifo vya watoto 87 kwa mwaka jana," alisema.

Alisema pia idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 77 kwa mwaka 2015 hadi kufikia vifo 17 kwa mwaka jana.

Kuhusu huduma ya maji, alisema mwaka 2015 upatikaji wa maji ulikuwa asilimia 52 pekee, lakini sasa huduma hiyo imeboreshwa baada ya kupata zaidi ya Sh. bilioni 4.3 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya miradi mikubwa sita ya maji.

Habari Kubwa