Halmshauri zashauriwa kufikiri upya

21Feb 2016
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe Jumapili
Halmshauri zashauriwa kufikiri upya

WASIMAMIZI wa fedha kwenye Halmashauri nchini wametakiwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitaziwezesha Halmashauri hizo kukusanya kodi yake katika mazingira yanayofaa bila kuleta kero kwa wananchi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Aidha, watendaji hao wametakiwa kuimarisha vyanzo vya mapato vilivyopo na kuangalia ni kwa namna gani serikali za mitaa zinashirikiana na serikali kuu katika ukusanyaji mapato.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Fedha wa Idara ya Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Shomari Mukhandi.

Mukhandi alikuwa akifungua mafunzo ya mipango na makadirio ya mapato ya vyanzo vya ndani vya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maafisa wa halmashauri, mikoa na Tamisemi.

Alisema watendaji hao wanapaswa kubuni vyanzo vichache lakini vyenye kuleta mapato ya kutosha katika Halmashauri zao, na pia visiwe kero kwa wananchi.

"Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo hivyo na pia kuzingatia kuwa mapato yake yanakusanywa katika mazingira yanayofaa," alisema Mukhandi.

Aidha, Mukhandi alisema watendaji wa halmashauri wanapaswa kuwa makini wakati wa kupanga mipango yao na kujiridhisha vyanzo hivyo mapato havileti bugudha kwa wananchi.

Hata hivyo, alisema serikali imekuwa na utaratibu wa kushirikiana na sekta binafsi katika shughuli za maendeleo na akapendekeza kuwa njia bora ya kuboresha ukusanyaji kodi ni kwa Mamlaka hizo kushirikiana na sekta binafsi.

Aliwataka watendaji hao kuzingatia mipango na bajeti pamoja na ukusanyaji na uandaaji wa taarifa za ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri.

Habari Kubwa