Halotel yasherehekea miaka 5 ya huduma

16Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Halotel yasherehekea miaka 5 ya huduma

RIPOTI ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ya robo ya pili ya mwaka imeonyesha Kampuni ya Viettel (Halotel), kufikia idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano zaidi ya milioni sita hadi kufikia Juni, mwaka huu.

Naibu Mkurugenzi wa Halotel, Nguyen Van Trung, akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya kampuni hiyo kwa maadhimisho ya miaka mitano ya utoaji huduma za mawasiliano nchini. Pembeni ni Ofisa Uhusiano, Stella Pius. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Halotel, jana imesherehekea miaka mitano ya utoaji huduma za mawasiliano nchini na kufikia malengo ya juu ikiwamo kuongeza watumiaji wa mtandao huo.

Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo ilisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa wa Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, pia Watanzania kwa ujumla ambao ni wateja wao, wafanyakazi wa Halotel pamoja na ubunifu wa kampuni hiyo kutengeneza huduma zinazokidhi na mahitaji ya watumiaji.

Akiongea na waandishi wa habari, Naibu Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Nguyen Van Trung, alisema; “Halotel imekuwa ikitoa huduma ya intaneti kwa shule za msingi na sekondari za serikali, imeunganisha mawasiliano kwa ofisi za serikali kuanzia ofisi za wilaya, vituo vya polisi na ofisi za posta kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufasaha.”

“Halotel ni mtandao wa kwanza kupeleka mawasiliano kwenye vijiji 4,000 ambavyo havikuwa na mawasiliano tangu Tanzania ilipopata uhuru na kusisimua maendeleo ya wakazi wa vijiji hivyo,” alisema Trung.

Alisema kama wawekezaji wengine Halotel imekuwa mstari wa mbele kwa kusaidia jamii kufikia maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwamo ya kiafya, elimu, mawasiliano, michezo, kilimo na watu wenye uhitaji maalumu kwenye jamii.

“Pia tunafurahia kuona Watanzania hivi sasa wameshika nafasi kubwa za uongozi (menejimenti) makao makuu na katika matawi yetu ya nchini. Haya ni mafanikio makubwa kuona kampuni inaendeshwa na kusimamiwa na Watanzania,” alisema Trung.

Katika kusherehekea miaka mitano, Halotel imezindua ofa maalum zitakazo wawezesha wateja wake kuwasiliana kwa punguzo kubwa. Hii ni mara ya kwanza kwa Halotel kutoa ofa kubwa kwa wateja wake na ofa hizo zinajulikana kama, “Dabo bando” na kuongea bure Halotel kwenda Halotel pia kwa wateja watakuwa wakipata zawadi mbalimbali ikiwamo vocha watakapo tembelea maduka ya nchi nzima ndani ya mwezi huu.

Pia, Trung alizindua ofa maalum ya Halopesa ya “kurudishiwa asilimia 50 ya makato ya kutuma pesa” kwa mtandao wa Halotel na mitandao mingine kwa muda wa siku tatu kuanzia Oktoba 15 hadi 17. Wakala na washirika wa Halopesa watapata zawadi na hati za shukurani.

Habari Kubwa