Hamasa kiwanda nyama ya punda

26Mar 2018
Elisante John
  SINGIDA
Nipashe
Hamasa kiwanda nyama ya punda

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya Singida, Eliya Dighah amependekeza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata nyama ya punda mkoani hapa, badala ya wanyama hao kupelekwa Dodoma kama malighafi.

NYAMA YA PUNDA

Mwenyekiti huyo alitoa pendekezo hilo kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC), kilichokutana mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Singida.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulijadili mikakati mbalimbali ya maendeleo ikiwamo uchumi wa viwanda.Dighah alisema punda wa Singida husafirishwa kwenda Dodoma, kilipo kiwanda cha kusindika nyama ya mifugo hiyo inayojulikana zaidi kwa kubeba na kuvuta mizigo, lakini ni wakati wa mkoa nao kuwa na kiwanda kama hicho.

Kiwanda cha nyama ya punda cha Huwa Cheng kipo Dodoma kikimilikiwa na wawekezaji kutoka China na Mei 31, 2016 Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) liliwahi kukifungia na kukitoza faini ya Sh. milioni 200 baada ya kubaini kinajihusisha na usindikaji wa nyama ya punda kinyume na utamaduni wa Watanzania huku mazingira yake yakiwa machafu.

Dighah alisema kiwanda hicho kinarudisha nyuma juhudi za mkoa katika suala la uwekezaji wa viwanda vipya mkoani Singida kwa kuifanya Singida kuwa mzalishaji wa malighafi.   

“Mheshimiwa Mwenyekiti kuna mnada wa Damankia Makiungu (Ikungi) ambao kwa wiki magari ya (Mitsubishi) Fusso mawili mpaka matatu yanabeba punda kupeleka kwenye kiwanda cha Wachina Dodoma," Dighah alisema na kupendekeza:

"Sasa (Wachina) wahamasishwe ili wajenge Singida na punda wachinjwe hapa hapa.”

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mkalama, James Mkwega alimpongeza Dighah kwa wazo hilo, akidai amedhihirisha wazi jamii ya eneo hilo ni watumiaji wakuu wa nyama ya punda, kutokana na kukiri hadharani kwenye kikao cha kamati ya ushauri.

Alisema kwa muda wa miaka mingi kumekuwa na mabishano juu ya nani hasa ni walaji wa punda kati ya jamii mbili za mkoa huo - Wanyaturu anakotoka Dighah na Wanyiramba (Mkwega) - lakini hivi sasa mjadala huo umefungwa rasmi kutokana na ombi la machinjio hayo.

Meya wa Manispaa ya Singida, Mbua Gwae, licha ya kupongeza wazo hilo alilodai ni muhimu kwa uchumi, aliomba zifanyike juhudi zaidi kusaka mwekezaji wa machinjio ya kuku wa kienyeji kuepuka kuwasafirisha na manyoya hadi jijini Dar es Salaam na maeneo mengine.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Eliasi Tarimo alisema pamoja na nia njema ya serikali ya awamu ya tano kuhusu uwekezaji wa viwanda, kiwanda cha nyama ya punda kinaweza kutowesha nguvu kazi ya wanyama hao wanaoelekea kuadimika.

Alisema takwimu za punda waliopo mkoani humo ni chini ya 38,000, na kwamba ujenzi wa kiwanda hicho ukifanywa kwa pupa utaathiri upatikanaji wa punda mkoani Singida siku za usoni kutokana na ongezeko la kasi ya kuwauza kwa ajili ya kitoweo litakalojitokeza.   

Mkoa wa Singida wenye halmashauri saba, una jumla ya viwanda 543 kikiwemo kikubwa kimoja, vya kati saba, vidogo 218 na vingine 317. Vimetengeneza ajira za kudumu 1,553.

Habari Kubwa