Hasunga, kigogo wa mbolea wateta

06Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Hasunga, kigogo wa mbolea wateta

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, jana alikutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Topic ya Cairo nchini Misri, Mhandisi Raouf Bakry jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga.

Katika kikao kazi kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Kilimo, Mhandisi Raouf, alimweleza Hasunga kuwa lengo la ziara yake ni kuangalia uwezekano wa kutumia fursa ya mkopo nafuu  inayotolewa na Benki ya Exim ili kufanya biashara kati ya nchi za Afrika.

Alisema akipatiwa mkopo huo, ataongeza uwezekano wa kusambaza mbolea na viuatilifu ili kuongeza tija na kasi ya uzalishaji wa mazao mbalimbali ya wakulima.

Hasunga kwa upande wake alimweleza Raouf kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya maendeleo ya viwanda, hivyo inawakaribisha wawekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwamo  viwanda vya kusindika mazao.

Alisema Rais Magufuli amejipambanua katika kuimarisha uwezekano wa wawekezaji kuwa na uwekezaji uliotukuka ili kuwanufaisha Watanzania sambamba na manufaa yao wenyewe.

Mkutano huo baina ya Waziri Hasunga Mhandisi Raouf, ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC), Salum Mkumba.