Hasunga sasa ataka kilimo hifadhi

04Jul 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Hasunga sasa ataka kilimo hifadhi

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesema ili Tanzania ifikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ni lazima iwekeze katika kilimo hifadhi na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa.

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga.

Hasunga aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akifungua warsha ya wadau wa kilimo hifadhi Tanzania.

 "Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki. Mfano tumefuta kodi nyingi lakini ni lazima tuhamasishane matumizi ya teknolojia za kisasa ambazo ni rafiki, ni muhimu tujadiliane pamoja kuruhusu sheria kwani hatuwezi kufika uchumi wa kati bila kufikia kilimo imara na chenye tija," alisema.

"Lazima kuimarishwe mafunzo kwani kilimo nchini bado kiko chini. Pia tuongeze utafiti kwa kuwa bila utafiti hakuna kilimo na lazima ijulikane kilimo gani kitumike, pembejeo gani zitumike, pia tuongeze uzalishaji wenye tija," aliongeza.

Hasunga pia alibainisha kuwa serikali inakuja na mkakati wa bima kwa wakulima lengo likiwa ni kumsaidia mkulima pindi mazao yake yatakuwa yanapoharibika shambani.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa, alisema kama serikali itawekeza katika kilimo hifadhi, sekta ya kilimo itafika mbali.

Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM) aliiomba serikali kuongeza bajeti katika sekta ya kilimo hasa katika utafiti.

Alisema matatizo yanayowakabili wakulima ni pamoja na masoko na miundombinu hivyo kuitaka serikali kuangalia sera na sheria zilizopo kwa kuwa nyingi zimetungwa wakati wa ukoloni.

"Sera na sheria zina matatizo makubwa unakuta mkulima natayarisha shamba, naanza kulima, napalilia halafu wakati wa kuvuna serikali inaanza kunipangia nikauze wapi. Hii si sawa kabisa hapa ni lazima tutengeneze sheria nzuri,” alisema Mgimwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kilimo Hifadhi Barani Afrika (ACT), Saidi Mkomwa, alisema kilimo hifadhi ni kilimo kinachozingatia uhifadhi wa rasilimali udongo na mazingira kwa ujumla.

Alisema kilimo hicho kimejengwa katika misingi mikuu mitatu ambayo ni kusumbua udongo, kuacha masalia shambani na kufanya kilimo mzunguko.

"Kilimo hiki ni cha miaka mingi na kilianza miaka 40 iliyopita Ulaya ila kwa barani Afrika bado kiko nyuma ndiyo kimefika sasa ila ni kilimo chenye faida na tija kubwa kwa mkulima," alisema Mkomwa.