Hatua nne kuzuia upotevu mapato zajatwa

29Jun 2022
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Hatua nne kuzuia upotevu mapato zajatwa

BUNGE limeelezwa hatua nne za kiukaguzi wa miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya kampuni za kimataifa kwa lengo la kuzuia upotevu wa mapato.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande, alitaja hatua hizo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina.

Katika swali lake, Mbunge huyo alihoji ni kwa kiwango gani serikali imejiimarisha kukagua miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya kampuni ya kimataifa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri alisema, serikali kupitia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhusu suala hilo.

Alitaja hatua hizo ni pamoja na kuendelea kuboresha mifumo ya ndani ya ukusanyaji kodi kama vile mfumo wa usimamizi wa mashine za utoaji wa risiti za kielektroniki na mfumo wa kuwasilisha ritani kielektroniki.

Pia alisema kutoa mafunzo ya vitendo kwa watumishi katika nchi mbalimbali zenye uzoefu wa kushughulikia miamala ya uhamishaji wa bei ya mauzo ya bidhaa na huduma baina ya kampuni za kimataifa.

Alibainisha kuwa kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa kubadilishana taarifa kati ya Serikali ya Tanzania na nchi zingine na kuendelea kufanya majadiliano na wadau mbalimbali ili kuona uwezekano wa kujiunga na Global Forum on Tax Transparency na ubadilishanaji wa taarifa kwa lengo la kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa.

Katika swali lake la nyongeza, alihoji maboresho hayo ni makubwa yamesaidiaje kuongeza kaguzi ikilinganishwa na zilizopita.

“Je, maboresho hayo yaliyofanywa na TRA yamesaidia kuokoa fedha kiasi gani zilizokuwa zikipotea kutokana na kukosekana kwa uwezo ndani ya nchi wa kukagua miamala hiyo?” Alihoji.

Chande akijibu maswali hayo, alisema maboresho hayo yameongeza asilimia 4.5 na kwa mwaka uliopita kabla ya maboresho ilikuwa asilimia 1.2.

Habari Kubwa