Hatua zaanza kukabili makali bei ya mbolea

21Jul 2021
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Hatua zaanza kukabili makali bei ya mbolea

SERIKALI imesema inatarajia bei ya mbolea kushuka katika siku chache zijazo, kutokana na shehena za mbolea takriban tani 25,000 kuanza kuingia kwa wingi nchini kuanzia mwezi huu.

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf  Mkenda, akizungumza akiwa bandarini Dar es Salaam jana, alisema kupanda bei kwa bidhaa hiyo kulitokana na uhitaji mkubwa wa mbolea katika nchi nyingi duniani kulikosababisha kupanda kwa bidhaa hiyo katika soko la dunia.

“Mbolea ilipanda kutokana na demand (uhitaji) wa bidhaa katika mataifa mbalimbali duniani, kwa hiyo baada ya nchi hizo kununua na kuanza kuitumia mbolea itakuwa na unafuu kwa sababu gharama ya uzalishaji wa mbolea haijapanda sana,” alisema Prof. Mkenda.

“Mimi kwa mfano nimetembelea kiwanda cha phosphate kule Morocco, gharama ziko pale pale kilichoongezeka ni wanunuzi wananunua kwa wingi… kwa hiyo bei ikapanda na wale wanunuzi mpaka mwezi wa nane hivi kati kati tunaamini watakuwa wameshachukua shehena wanayohitaji, hivyo bei itashuka,”aliongeza.

Alisema kutokana na kuingia kwa wingi kwa mbolea, ambayo waagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi wameshaagiza, na kuondolewa kwa urasimu wa uagizaji katika mfumo wa uagizaji wa pamoja na kuruhusiwa kila mwenye uwezo kuagiza mwenyewe, ni matarajio ya Serikali kuwa bidhaa hiyo sasa itashuka bei kuliko ilivyo sasa.

Akizungumzia shehena za mbolea zinazotarajiwa kuingia, Kaimu Meneja wa Sehemu ya Kichele bandarini hapo inayohusika na bidhaa za kichele kama mbolea,  Tatu Moyo, alisema wanatarajia kupokea  tani 11,000 ya mbolea aina ya granula,  Jumapili kutoka kampuni ya ETG ,  Julai 29, mwaka huu tani 4,753 ya mbolea aina ya granula , Julai 31mwaka huu tani 9,400 ya mbolea aina ya CAN.

Akizungumza na waagizaji na wasafirishaji wa mbolea mwishoni mwa wiki , Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema Wizara hiyo ina mpango wa kuzungumza na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ili kupunguza bei za usafirishaji wa bidhaa hiyo kutoka kwa wafanyabiashara kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.