Hekari 25 za mashamba ya bangi zagunduliwa, yateketezwa moto

19Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Hekari 25 za mashamba ya bangi zagunduliwa, yateketezwa moto

ZAIDI ya hekari 25 za mashamba ya bangi zimefyekwa na kuteketezwa kwa moto katika kitongoji cha Nembwibwi, kijiji cha Kijungumoto, kata ya Mashewa, wilayani Korogwe, katika operesheni inayoendelea ya kutokomeza dawa za kulevya.

Tukio hilo lilifanyika juzi likiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Robert Gabriel, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Usalama wilayani humo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, taarifa za kuwapo kwa mashamba hayo zilitolewa na wasamaria wema na kwamba wahusika na bangi hiyo wanasakwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Korogwe, Gabriel alisema operesheni hiyo itakuwa endelevu lengo likiwa ni kutokomeza kabisa bangi na dawa nyingine za kulevya wilayani humo.

Mkuu huyo wa wilaya alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji hasa wevyeviti na watendaji kutokutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha vita dhidi ya dawa za kulevya na kuonya kwamba kuanzia sasa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

"Inashangaza kuona bangi ikilimwa kwa wingi tena kwa muda mrefu kwenye baadhi ya maeneo huku viongozi hao wakidai kukosa taarifa juu ya uwepo wa mashamba hayo, mazingira ambayo yanatia wasiwasi juu ya uadilifu wao."

"Hii haitawezekana, kuanzia sasa kiongozi ambaye atashindwa kutoa taarifa kama eneo lake kuna shamba la bangi ama kuna jambo lolote haramu linaendelea tutamchukulia hatua kali za kisheria, inawezekanaje kiongozi ndani ya eneo lake la utawala hajui
kinachoendelea," alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo baada ya kuomba kutajiwa wahusika wa mashamba ya bangi katika kitongoji cha Nembwibwi lakini kila kiongozi aliyemuuliza alidai hakuwa akifahamu kama kulikuwa na kilimo hicho katika eneo lake.

Habari Kubwa