H/shauri zaelekezwa mazao ya nyuki

25Feb 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
H/shauri zaelekezwa mazao ya nyuki

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameagiza kuboreshwa kwa sekta ya misitu na mazao ya nyuki na kuhakikisha kila halmashauri inakuwa na kiwanda cha kuchakata mazao hayo ya nyuki na kuviboresha zaidi vile vya uzalishaji wa mazao ya mbao.

Amesema lengo ni kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao ya misitu na nyuki nchini.

“Viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki kwa sasa vipo 21, lakini wizara imeongeza viwanda vitatu kwa hiyo tutakuwa na viwanda 26 ambavyo bado havitoshi, katika hali ya kawaida hivi viwanda vidogo tunatakiwa tuwe navyo 200,” alisema Samia.

“Tuna halmashauri 186, kwa hiyo kila halmashauri ikiwa na kiwanda kimoja ambacho nacho hakitoshi lakini itakuwa angalau.”

Samia alitoa maagizo hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, wakati wa uzinduzi wa kongamano la kimataifa la sayansi juu ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki kwa ajili ya maisha endelevu na uchumi wa viwanda.

Alisema kuwa kuna haja ya kuwa na mkakati mahsusi wa kuainisha masoko na tabia zake katika kufanikisha sekta hiyo na kutaka utafiti unaofanyika  uwafikie wadau na uandikwe kwa lugha nyepesi.

“Tanzania ina wasomi wengi sana na wanafanya utafiti, katika mazao ya nyuki na misitu, hakuna taasisi nzuri za utafiti Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara kama za Tanzania, lakini tafiti nyingi zinawekwa kwenye makabati, ni wakati sasa tafiti zifike kwa wadau katika jamii zetu, na kuziandika katika lugha nyepesi,” alisema Samia.

Alisema bado nchi haijatumia vizuriraslimali hizo za misitu na nyuki na kwamba kuna haja kuliangalia hilo.

“Uwezo wa nchi wa kuzalisha asali ni tani 134,000, lakini kwa sasa tunazalisha tani 34,000 tu, tunataka mtuambie nini kifanyike ili twende mbali zaidi,” alisema.

Samia aliagiza kila halmashauri nchini kuhakikisha inapanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Pia, aligiza kuongeza jitihada katika kusimamia uhifadhi na utunzaji wa mazingira hususani ukataji wa miti.

“Endapo miti yote itakatwa halafu oksijeni itengenezwe kwenye maabara ambayo thamani yake ni Sh. 22.7 kwa mwaka mzima, ni watanzania wangapi wanaweza hilo, watu tutakufa, ndio maana nawaagiza msikate miti kwa sababu hatuna fedha ya kununua hiyo oksijeni ya maabara,” alisema Samia.

Aliagiza kuthibiti mifugo na shughuli za kilimo kwenye hifadhi za misitu na kulitaka Jeshi Usu kuhakikisha linathibiti hilo.

Naibu Waziri wa Masiali na Utalii, Mary Masanja, alisema sekta ya ufugaji na nyuki imeonyesha kuwa inaweza kuchangia sehemu kubwa katika ukuaji wa uchumi.

Alisema wizara imechukua hatua ya kuboresha uzalishaji, uchakataji biashara za mazao ya nyuki ili kuhakikisha inaongeza zaidi pato la taifa.

Habari Kubwa