Huduma wezeshi kwa wakulima mbioni

15Feb 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Huduma wezeshi kwa wakulima mbioni

WIZARA ya Kilimo imesema inaangalia namna ya kuwapo na huduma wezeshi kwa wakulima kutambua aina ya udongo na mbolea inayopaswa kutumika shambani.

Naibu Waziri wa Wizara ya kilimo, Hussein Bashe, picha mtandao

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hussein Bashe, alipokuwa akizungumza katika Kongamano la Sita la Jukwaa la wadau wa sera za kilimo, mifugo na uvuvi, jijini hapa.

Alisema tatizo ambalo wizara hiyo inakabiliana nayo ni namna ya kufanya utaratibu huo kama huduma kwa mkulima ambayo ataweza kumudu.

“Kwa mfano, ukichukua sampuli moja ukaenda kwenye kituo cha utafiti unapaswa kulipa kiasi cha Sh.100,000 kwa mkulima mwenye hekari 5-10 anataka kuchukua sampuli zaidi ya moja atapaswa kutumia kiasi gani?” alihoji.

Alisema suala hilo linajadiliwa ndani namna ya kufanya utaratibu huo kama huduma kwa sekta ya kilimo.

Akizungumzia kuhusu nzige, Bashe alisema Tanzania bado haijashambuliwa na nzige na hakuna eneo lolote lililoshambuliwa.

“Tumejipanga kwa vifaa na dawa, tunawaomba nyie kama wadau muanze kujadili namna ya kushirikiana kupambana na suala hili,” alisema.

Aliwaomba kutumia washirika wenzao kwenye nchi zilizokumbwa na nzige ili kujua namna walivyofanikiwa kupambana nao.

“Hatua hii itasaidia serikali kupata taarifa ili kujipanga vyema na kujua namna ya kukabiliana nao ili wasilete madhara,” alisema.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utafiti kuhusu zao la kahawa, Mkurugenzi wa Jukwaa la wadau wa kilimo wasio wa kiserikali(ANSAF), Audax Rukonge, alisema lazima kutangaza uwekezaji kwenye zao hilo ili kuleta ushindani na kuondoa kero zinazowakabili wakulima.

“Pia badala ya msimu wa kahawa kufunguliwa na kufungwa, iuze mwaka mzima ili wakulima waamue ni lini wauze kahawa zao,”alishauri.

Nao, baadhi ya wadau wakichangia kwenye kongamano hilo, walitaka kuwapo na mnyororo wa thamani kwenye zao la alizeti ili kuongeza uzalishaji nchini wa mafuta.

Habari Kubwa