Jafo atoa miezi sita ujenzi wa hospitali kukamilishwa

17Jul 2019
Augusta Njoji
CHAMWINO
Nipashe
Jafo atoa miezi sita ujenzi wa hospitali kukamilishwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesisitiza Hospitali ya Uhuru  wilayani Chamwino kujengwa na kukabidhiwa kwa serikali ndani ya miezi sita kuanzia sasa.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo.

Hospitali hiyo inajengwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi (SUMA JKT). Jafo aliyasema hayo baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa hospitali hiyo ikiwa ni mara ya pili kutembelea eneo hilo.

 

"Juni 16, mwaka huu nilitembelea eneo hili na kukuta pori kukiwa hakuna kitu kinachoendelea, kutokana na hali hiyo nilitoa maagizo ya kuanza mara moja ujenzi na ufanywe na moja ya vikosi vya majeshi na ukamilike ndani ya miezi sita,

 

"Kwa kweli kwa hatua za awali nimeridhishwa na kazi hii, nimekagua eneo la ekari 40 limesafishwa vizuri, mabati yamezungushwa, eneo la kuhifadhia vifaa limejengwa… hii inaonyesha maandalizi ya awali ya ujenzi huu yameanza, kwa kweli mmenifurahisha, wiki yangu imeanza vizuri,” alisema Jafo.

 

Alisema anataka hospitali hiyo ikamilike Januari mwanzoni mwaka 2020 kwa ubora unaotakiwa.

 

Jafo aliwataka watendaji walio chini ya wizara yake kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea, na kutaka kutekeleza wajibu wao bila kusukumwa sukumwa.

 

"Niwaombe wataalamu wangu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na tunapotoa maagizo basi wayatekeleze kwa wakati, ni matarajio yetu hadi kufikia Januari, 2020 tutakuwa tumeshakamilisha ujenzi huu.”

 

Alieleza kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo itakuwa ni kutimiza azma ya Rais John Magufuli katika kutoa huduma bora za afya karibu na wananchi.

 

Naye msanifu Daneil Mwakasungura kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao ndio washauri na wasimamizi wa mradi huo, alisema mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi walioingia na SUMA JKT unagharama ya Sh. bilioni 3.

 

Alisema awamu hii itahusisha ujenzi wa jengo hilo litakalokuwa la ghorofa moja utajumuisha majengo ya wagonjwa wa nje, X-ray, maabara, kliniki ya mama na mtoto, meno na macho.

 

“Tunachosubiri hapa ni SUMA JKT kutupa ratiba ya kazi ambayo ndiyo itatuongoza nini cha kufuata, ila makubaliano yetu ni kuwa ujenzi wa awamu ya kwanza unafanyika kwa mwezi sita na Januari 10 mwakani, jeshi linatakiwa kukabidhiwa kwa serikali.

 

“Tayari mkandarasi aliyepewa kazi amenza maandalizi ya awali ya ujenzi, ikiwa ni kujenga ofisi, uzio, eneo la mradi limesafishwa kwa kuondoa miti na udongo umeshachukuliwa na kupimwa.”

 

Mwakasungura alisema mchoro unaotumika ni ule wa Tunduma, lakini wataalamu wa wizara ya Tamisemi na Wizara ya Afya na mkoa wamefanya maboresho kwa baadhi ya huduma kwa kuzishusha chini na utawala kuwekwa juu.

 

Pia Mwakasungura alisema awamu ya pili ya ujenzi wa hospitali hiyo ambao utafanyika baada ya fedha zingine kupanikana utahusu jengo la dharura, chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) na wodi.

Naye msimamizi wa ujenzi wa SUMA JKT kutoka Kanda ya Ziwa, Luten Kanali, Onesmo Njau, alisema wamekabidhiwa kazi Juni 19 mwaka huu, na kwa sasa wameshaanza maandalizi ya awali.

 

"Niwahakikishie kuwa sisi hatuna shida tutatekeleza mradi huu kwa wakati na kwa ubora, jambo la msingi hapa ni fedha kutolewa kwa wakati.”