Japan, Tanzania zahimiza kilimo cha mboga

22Jun 2016
Lulu George
Tanga
Nipashe
Japan, Tanzania zahimiza kilimo cha mboga

SERIKALI ya Japan kwa kushirikiana na Tanzania imewahimiza wakulima wa mazao ya mboga na matunda wilayani Lushoto kuongeza uzalishaji ili kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yao kwa soko la ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella

Rai hiyo ilitolewa na ujumbe wa viongozi wa serikali ya Japan na Tanzania walipokwenda katika Kijiji cha Buheloi, Kata ya Gale wilayani Lushoto kukagua miradi ya kilimo inayosimamiwa na shirika la maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) na kisha kuzungumza na wakulima hao.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella ambaye alisema serikali itawaunganisha wakulima na wageni wa mataifa mbalimbali ili waweze kupata masoko yenye tija.

“Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa wilaya maarufu kwa kilimo cha mboga na matunda hapa nchini kama serikali tunapaswa kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha soko la mazao haya, lakini tunahitaji ushirikiano kutoka kwa wakulima ili kwa pamoja tuweze kufanikisha azma hiyo, lakini uzalishaji unatakiwa kuongezeka maradufu,” alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Jica nchini, Toshio Nagase, aliahidi kutangaza soko la mazao yanayozalishwa na wakulima wa Wilaya ya Lushoto, katika hoteli mbalimbali za kimataifa zilizopo Tanzania na Japan.

“Mimi ni waahidi tu kwamba tutahakikisha tunaongeza utangazaji wa kilimo hiki katika hoteli za Tanzania na Japan ili mazao yenu yawe na soko la uhakika wa ndani na nje ya nchi,” alisema.

Kufuatia hatua hiyo Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wilayani Lushoto, Dk. Hassan Shelukindo, alisema wameanza operesheni ya kuwakamata baadhi ya mawakala wanaowauzia mbegu feki wakulima ili azma iliyowekwa na serikali ya kuuza mazao hayo kwa tija katika masoko ya kimataifa iwezekane.

“Wapo mawakala wa mbegu ambao wamekuwa wakiwatia hasara wakulima katika misimu ya mavuno na matokeo yake kuvuna kile ambacho hawakikutarajia na hata mazao yenyewe kutoka katika ubora unaoweza kushindanishwa kwenye soko hii hali ni mbaya na tunahakikisha tutawafungioa wote wanaosambaza mbegu zisizo na ubora,” alisema.

Habari Kubwa