Jela yanukia wahusika pembejeo za ruzuku

25Nov 2018
Gurian Adolf
Mpanda
Nipashe Jumapili
Jela yanukia wahusika pembejeo za ruzuku

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Katavi imeahidi kuwapandisha kizimbani baadhi ya wazabuni waliosambaza pembejeo za kilimo za ruzuku msimu wa kilimo wa mwaka 2015/16.

Hatua hiyo inachukuliwa baada ya kubaini kuwa wamefanya udanganyifu wakati wakisambaza pembejeo hizo kwa wakulima.

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoa huo Christopha Nakua, wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa tasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.

Alisema kuwa Takukuru itakapokuwa imekamilisha kazi ya uhakiki wa madai ya wazabuni wote ambayo yalikuwa ni jumla ya Shilingi bilioni 3.8 ambayo mpaka sasa uchunguzi umebaini kuwapo kwa udanganyifu mkubwa.

Alisema baada ya serikali kuagiza madai ya wazabuni hayo yahakikiwe ndipo waweze kulipwa anaamini kiwango hicho kitapungua kutokana na wadanganyifu kubainika.

Nakua alisema kuwa wakati wakiendelea kufanya uchunguzi imebainika kuwa kuna baadhi ya wazabuni walikuwa wakifanya udanganyifu kwa kujiongezea kiwango kikubwa cha fedha tofauti na kazi waliyofanya.

"Lazima wazabuni hao wasio waaminifu wawajibishwe kwa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, kwani hawawezi wakaachwa kwa kuwa nao wanajua fika kitendo walichofanya kilikuwa ni kosa kisheria" alisema.

Nakua aliongeza kuwa hatua hiyo itakuwa fundisho kwa baadhi ya wazabuni ambao wamekuwa si waaminifu wenye lengo la kutaka kuiibia serikali na hiyo itasaidia mchezo huo kuisha kwani ulikuwa umeota mizizi kwa baadhi yao sasa imefika wakati lazima ukomeshwe.

Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Katavi alisema kuwa tasisi hiyo inaendelea na uchunguzi wa miradi mbalimbali ya maji na itaendelea kuujulisha umma kadri uchunguzi utakavyo kuwa unaendelea.

Lengo lao ni kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa thamani ya fedha kulingana na mradi ili wananchi wapate huduma ya maji kama ilivyo kusudiwa.

Alifafanua kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi cha miezi mitatu Takukuru mkoa imepokea malalamiko ya vitendo vya rushwa 35 na kufungua majalada matano ya uchunguzi.

Alieleza kuwa katika kuelimisha umma wameyafikia makundi mbambali kwa lengo la kuyaongezea ufahamu wa kutosha katika masuala ya rushwa ili wawe mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa.

Aliwataka baadhi ya wazabuni kubadilika na kuacha tabia ya kufanya kazi kwa ujanja na uongo kwani zama hizo zimepitwa na wakati.

“Ni lazima kila mmoja kuwa na uchungu na mali ya umma na waache dhana ya kuamini kuwa mali ya umma haina mwenyewe tofauti na hivyo wengi watajikuta wakikabiliwa na mkono wa sheria.”

Habari Kubwa