JICA wafanya ziara ya mafunzo TBL

14Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
JICA wafanya ziara ya mafunzo TBL

WATAALAM wa fani mbalimbali kutoka Shirika la Maendeleo la Japan la (JICA) wamefanya ziara katika kiwanda cha kutengeneza Bia cha Dar es Salaam kilicho chini ya kampuni ya TBL Group ili kujifunza mbinu bora za uendeshaji viwanda zenye kuleta tija na mafanikio.

Katika ziara yao hiyo ya mafunzo iliyofanyika hivi karibuni, waliweza kuona hatua mbalimbali za uzalishaji wa vinywaji unaofanywa na kiwanda cha kutengeneza bia cha TBL na kuelezwa mikakati ya viwanda vilivyopo chini ya TBL Group hapa nchini ambavyo viko katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.

Meneja wa Kiwanda cha Kutengeneza bia cha Dar es Salaam, Calvin Martin aliwaeleza kuwa mafanikio ya viwanda vilivyo chini ya TBL Group nchini yanatokana na mikakati madhubuti iliyowekwa na kampuni mama inayomiliki viwanda hivyo ya SABMiller.

Alisema uendeshaji wa viwanda hivyo unafuata miongozo, mikakati na sera zilizowekwa na kampuni mama ya SABMiller ambayo inaleta tija na ufanisi ikitekelezwa ipasavyo kwa kuwa ina mwelekeo wenye uzalishaji unaolenga kwenye uzalishaji bora na wa viwango vya kimataifa.

Martin alisema hatua hiyo inaambatana na kujali maslahi ya wafanyakazi, kujali utunzaji wa mazingira kwenye viwanda na maeneo vilipo, kuzingatia kanuni za mahesabu na kulipa kodi za serikali, kuzingatia kanuni za usalama kazini, kuzingatia taratibu za ajira na kuinua maisha ya watu wanaoishi maeneo vilipo viwanda ikiwamo kusaidia wazalishaji wa malighafi zinazotumiwa na viwanda vyake .

"Miongozo ya kampuni mama ya SABMiller ikitumika popote na watumiaji kwa kuizingatia, lazima matokeo mazuri yapatikane na ndio maana viwanda vilivyopo chini ya TBL Group ni kioo cha sera ya uwekezaji nchini kwa kuwa mbali na kuongoza kuchangia pato la serikali kwa kulipa kodi serikalini, kutengeneza ajira pia inanufaisha wananchi kwa njia mbalimbali na hii inatokana na kuwa na mfumo mzuri na utekelezaji wake kufanyika vizuri.”alisema Martin.

Habari Kubwa