Jiji Dar, NBC wawapa elimu wajasiriamali

17Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Jiji Dar, NBC wawapa elimu wajasiriamali

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), wameendesha mafunzo ya biashara,  elimu ya fedha na mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali vijana, wanawake na wenye ulemavu waliopo katika jiji hilo.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa ili waweze kutumia vema mikopo na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali pamoja na jiji hilo.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo yaliyowakutanisha  pamoja wajasiriamali zaidi ya 400, Ofisa Maendeleo ya Vijana kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Sapiencia Masaga pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa jitihada hizo,
alisema  mafunzo hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa wajasiriamali hao kutumia vyema mikopo wanayoipata kutoka serikalini na halmashauri za jiji hilo ili kujikwamua kiuchumi kulingana na malengo ya mikopo hiyo.

“Licha ya jitihada kubwa inayofanywa na halmashauri zetu kwa kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali vya vijana, kinamama na wenye ulemavu bado tumekuwa hatupati matokeo mazuri sana kwa sababu wengi wa walengwa wamekuwa wakishindwa kutumia vema mikopo husika na matokeo yake wanashindwa kufikia malengo na zaidi wanashindwa kufanya marejesho. Tunawashukuru NBC kwa kuwa mafunzo haya yanalenga kuondoa hiyo changamoto,’’ alisema.

Meneja Ukuzaji Biashara wa NBC, Isdory  Sebastian, alisema benki hiyo imeshirikiana na Halmashauri ya Jiji la Ilala katika kutoa mafunzo hayo ili kujenga uelewa wa kutosha kuhusu usimamizi bora wa kifedha, umuhimu wa bima mbalimbali ikiwamo za afya na biashara pamoja na namna bora ya kutunza akiba zao waweze kuendesha shughuli zao kitaalamu waepukane na hasara inayoweza kukwamisha ustawi wa biashara zao.

“Katika mafunzo hayo Benki ya NBC tumejitahidi kuhakikisha walengwa wanajengewa uelewa wa kutosha ili sisi kama benki tusiishie tu kuwahifadhia fedha zao wanapokopeshwa na hizi halmashauri bali pia tuwasaidie kuhakikisha hiyo mikopo inakuwa na tija kwa pande zote yaani halmashauri na wajasiriamali.’’

“Tunawashukuru sana Manispaa ya Ilala tungependa na halmashauri nyingine pia waige mfano huu kwa sababu mikopo hii inahitaji elimu sahihi kwa walengwa ili waweze kujikwamua kutoka kwenye umaskini na zaidi pia waweze kurejesha hizo fedha zitumike kuwakopesha wahitaji wengine,’’ alisema.

Wajasiriamali Iddy Kaziulaya na Bahati Angetile walisema mafunzo hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwajengea uwezo wa kibiashara kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakishindwa kuendeleza vema mikopo hiyo kulingana na malengo kusudiwa, hali inayochangiwa na kukosekana kwa elimu ya kutosha katika uendeshaji wa shughuli zao.