Jiji kukusanya bil. 74.9/- mwaka 2021/2022

22Feb 2021
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Jiji kukusanya bil. 74.9/- mwaka 2021/2022

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya inakusudia kukusanya zaidi ya Sh. bilioni 74.9 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwamo makusanyo ya kodi.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Amede Ng’wanidako, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji hilo la kujadili makadirio ya bejeti ya mwaka ujao wa fedha.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 16.6 ni mapato ya ndani Sh. bilioni 49.5 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Halmashauri, Sh. bilioni 1.6 ni fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 3.5 ni fedha za miradi.

Aidha alisema Halmashauri hiyo inatarajia kupokea Sh. bilioni 2.8 kwa ajili ya elimu na malipo na michango ya wananchi inatarajiwa kuwa Sh. bilioni 1.2 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Tunachoomba ni ushirikiano kutoka kwa madiwani kwenye makusanyo ya fedha hizi ili tufanikishe bajeti hii, endapo hatutafikia malengo haya kuna hatari wananchi wakakosa imani na sisi maana tunakusanya kwa ajili ya maendeleo yao,” alisema Ng’wanidako.

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo waliiomba Menejimenti kuhakikisha bajeti hiyo inatekelezwa kama ilivyopangwa ili kubadili sura ya Jiji.

Hamphrey Ngalawa, Diwani wa Kata ya Iwambi, alisema watendaji wa Halmashauri wanatakiwa kujipanga na kuhakikisha wanakusanya mapato na kuyaelekeza kwenye bajeti hiyo ili wananchi waamini kile wanachoambiwa.

Alisema wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, madiwani hao pamoja na wabunge waliwaaminisha wananchi kuwa wakiwachagua watawapelekea maendeleo na kwamba wananchi wanachosubiri ni utekelezaji.

Alisema vipaumbele ambavyo vimewekwa kwenye bajeti hiyo vinaendana na kilichomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo ndio mkataba kati ya Serikali na wananchi.

“Niwaombe watendaji wa Halmashauri yetu, wasipindishe bajeti hii maana inajibu vizuri mahitaji ya wananchi wetu ambao ndio waliotutuma tuwawakilishe, sisi tukitoka hapa tunaenda kuwaaminisha wananchi wetu kuwa tumepanga hiki,”  alisema Ngalawa.

Mary Malema, Diwani wa Viti Maalumu, alisema katika bajeti hiyo moja ya vipaumbele muhimu ni kuboresha miundombinu ya elimu ikiwamo ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo kwenye Shule za Msingi na Serondari.

Habari Kubwa