Jiko kupunguza matumizi mkaa

17Jul 2019
Beatrice Philemon
Dar es Salaam
Nipashe
Jiko kupunguza matumizi mkaa

CHUO cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha Moshi mkoani Kilimanjaro kimetengeneza jiko linalotumia gesi ili kupunguza matumizi ya mkaa.

MKAA.

Malengo mengine ni kupunguza uharibifu wa uoto wa asili, kulinda afya za wapishi, kuongeza ufanisi wa upikaji na kutumia gesi ndogo kuliko kuni.

Akizungumza na Nipashe hivi karibuni katika maonyesho ya Sababasa, Mwalimu wa Ufundi, John Nathan, alisema wameamua kutengeneza jiko hili ili kwendana na mpango wa serikali kuondoa vitu vinavyoharibu hali ya hewa na kuharibu uoto wa asili.

Hadi sasa chuo hicho kimetengeneza majiko manne yanayotumia gesi yenye uwezo wa kupika kilo 20-25 za wali, ambao waliupeleka kama sampo katika maonyesho ya mwaka huu, ili kutangaza bidhaa hiyo, na pia kusaidia wananchi kupunguza matumizi ya mkaa, hivyo kuanza kutumia gesi katika shughuli zao za mapishi.

“Tunashukuru Mungu mwitikio wa matumizi ya majiko haya umekuwa mzuri, tumepata oda nyingi kwenye shule na taasisi mbalimbali kutoka mkoa wa Dar es Salaam, Shinyanga ikiwamo wakala wa gesi,” alisema.

Alisema majiko haya yametengenezwa na wanafunzi kwa kushirikiana na walimu kupitia programu ya mafunzo.

“Majiko haya yanapunguza gharama ya kupika kwa mfano, unaweza kutumia kilo 1.5 ya gesi kwa ajili ya kupika chakula ambacho ni gharama ndogo,” alisema.

Pia chuo hicho kina mpango wa kusambaza majiko hayo nchi nzima kwenye shule, magereza, hotelini, hosptalini ili watumie gesi badala ya kuendelea kutumia mkaa ambao unachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

“Ukizunguka katika maeneo mbalimbali nchini, tatizo linalokabili suala la mazingira, ni matatizo ya mabadiliko ya tabianchi na tatizo mojawapo ni ukataji wa misitu kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo uchomaji mkaa, shughuli za kilimo, upasuaji mbao na utafutaji kuni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.”

Matumizi ya mkaa yameongezeka sana na takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania inatumia tani milioni 2.5 kwa mwaka na asilimia 60 ya mkaa huo unatumika Dar es Salaam.