JPM aionya TRA uonevu ukadiriaji viwango kodi

03Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe
JPM aionya TRA uonevu ukadiriaji viwango kodi

RAIS John Magufuli, amewaonya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), dhidi ya uonevu unaofanywa na baadhi yao kwa kuwakadiria wafanyabiashara viwango vikubwa vya kodi, hali ambayo inawafanya wakwepe kulipa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Meya wa jiji la Arusha Kalist Lazaro mara baada ya kuwahutubia wananchi wa Arumeru.

"Kweli kabisa, kodi zingine TRA zinaudhi kweli...wanatoa makadirio ya juu sana na wengine wakienda kukusanya kodi hizo, wanasema, 'Hapa Kazi Tu.' Hivi kweli niliwatuma kukusanya kodi za namna hiyo? Watu wa namna hiyo hawana nafasi katika serikali hii," alisema.

Alisema hayo wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi mkubwa wa maji katika chanzo kilichopo eneo la Kimnyak, wilayani Arumeru jana.

Mradi huo utakapokamilika utatoa lita milioni 208 za maji kwa siku na hivyo, kumaliza tatizo kwa wakazi wa Jiji la Arusha na vijiji saba ambavyo bomba  litapita.

Alisema mahitaji ya maji kwa wakazi wa Jiji la Arusha ni lita milioni 94 kwa siku.

Alisema fedha za mradi huo Sh. bilioni 520 zimekopwa kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na zitalipwa na Watanzania wote kama ambavyo Arusha pia inalipia fedha zilizokopwa kwa ajili ya miradi inayotekelezwa katika mikoa mingine na hiyo ndiyo maana ya maendeleo kwa kuwa hayana chama.

"Tumekopa fedha hizi kwa ajili ya wanyonge, ambao wameteseka mno," alisema Rais Magufuli na kuongeza: "Hatutakopa fedha kwa miradi ambayo haitakamilika...ni lazima fedha tunazokopa zikaonyeshe matunda mazuri ya kazi iliyokusudiwa."

Akizungumzia zaidi kuhusu TRA, aliwahisi pia Wizara ya Fedha, kuweka 'fair play' (usawa) katika makadirio ya viwango vya kulipa kodi, ambavyo alisema baadhi ni vikubwa na watu wanakwepa kulipa kodi au kuwakimbia.

"Ni bora kuweka makadirio ya viwango vidogo vidogo vya kodi vinavyoweza kulipika badala ya kuweka viwango vikubwa vinavyowafanya watu waanze kukwepa kulipa kodi.

Aidha, Rais Magufuli aliitaka TRA kufanya utafiti kwa nini watu wanakwepa kodi, au inaweza wakati mwingine sababu ikawa wao.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli, alionyesha kusikitishwa na baadhi ya watu wanaowatumia wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) kwa kuwapa bidhaa za fedha nyingi waziuze mitaani kwa lengo la kukwepa kodi.

Alitaka wafanyabiashara hao kuwafichua wanaokwepa kodi kwa mtindo huo.

"Ninasikitishwa na baadhi wanaoanza kuwatumia wafanyabiashara ndogondogo kukwepa kodi, wapo wanaowachukua wafanyabiashara kwa mfano, 10 hivi na anawapa bidhaa kila mmoja asubuhi akaziuze. Wapo pia ambao hawatumii mashine za kielektroni za kutolea risiti (EFDs).

"Ninawaomba wamachinga, wasikubali kutumika kukwepa kodi...serikali iliwaruhusu kufanya biashara mbalimbali sasa wasitumie fursa hiyo kwa kukwepa kulipa kodi. Hapo tunakwenda kubaya na serikali yoyote isiyokusanya kodi (mapato) ni mufilisi," alisema.

Akijibu kero ya barabara na umeme, Rais Magufuli aliamua kuipandisha hadhi barabara kuanzia eneo la Mianzini Kimnyak hadi Ngaramtoni, yenye urefu wa kilomita 18 kutoka chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), hadi kuwa mali ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Alisema fedha zilizotengwa na Tamisemi kwa ajili ya ujenzi huo zitaongezwa na zile za Tanroads na mchakato wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami uanze baada ya kukamilika kwa taratibu za upembuzi yakinifu na masuala mengine yahusuyo ujenzi wa barabara.

Kuhusu umeme alisema mkarandasi aliyepata zabuni ya kusambaza umeme wa REA anapaswa kuangaliwa kama uwezo wake upo vizuri au la na kama hawezi basi apewe mkandarasi mwingine.

Mapema Mkurugenzi Mkazi wa AfDB nchini, Dk. Alex Bubiru, alisema wataendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye maslahi kwa taifa.

Alisema mradi huo wa maji utawawezesha wananchi kutopoteza muda mrefu kutafuta maji yanayopatikana umbali mrefu na kwamba hakuna mwanafunzi atakayeshindwa kwenda shule kwa sababu amekosa maji.

Alisema mradi huo umeonyesha ushirikiano mzuri uliopo kati ya serikali ya Tanzania na AfDB.

 

 

Habari Kubwa