JPM, wafanyabiashara kujadiliana Ikulu leo

19Mar 2018
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
JPM, wafanyabiashara kujadiliana Ikulu leo

RAIS John Magufuli, leo atakutana na wafanyabiasharanchini kwa ajili ya kujadili mafanikio na changamoto katika Mkutano wa 11 wa Baraza Taifa la Biashara (TNBC).

RAIS John Magufuli.

Mkutano huo ambao utaongozwa na Rais kama Mwenyekiti wa Baraza, utafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu, jijini Dar es Salaam.

 Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Raymond Mbilinyi, kwa vyombo vya habari jana, maandalizi ya mkutano huo yameshakamilika na wajumbe wote wamethibitisha ushiriki wao.

 

“Huu ni mkutano muhimu sana kwa sekta za umma na binafsi kwani unatoa fursa kwa pande mbili hizi kujadiliana namna bora ya kujenga mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji zaidi nchini,” alisema Mbilinyi.

 

Alisema  mkutano  wa 11 wa baraza utakuwa wa pili kuuongozwa na Rais Magufuli kama Mwenyekiti wa Baraza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano.

 

“Mkutano huu unafanyika wakati kukiwa na mafanikio makubwa chini ya awamu ya tano ikiwamo viwanda zaidi 3,500 vimeshaanzishwa katika kipindi kifupi,” alifafanua.

 Kwa mujibu wa Mbilinyi, serikali ya awamu ya tano imesimamia mabadiliko mbalimbali yaliyolenga kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa kati na viwanda.

 “TNBC ni jukwaa pekee la majadiliano ambalo hutoa fursa kwa sekta binafsi Tanzania kujadiliana moja kwa moja na serikali kuhusu masuala ya kipaumbele kwa uchumi na ustawi wa maendeleo ya taifa,” alisisitiza.

 Alisema kupitia mabaraza ya biashara ya mikoa (RBCs) na yale ya wilaya yaani DBCs chini ya uwenyekiti wa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya yameweza kuhamasisha na kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi na maendeleo katika maeneo husika.

 

TNBC ni chombo muhimu cha majadiliano kati ya sekta za umma na binafsi ambacho hutoa fursa pekee kwa viongozi kutoka pande hizo mbili kuhusu mambo mbalimbali namna ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini pamoja changamoto zake.

 

Kimuundo baraza lina wajumbe idadi sawa kutoka sekta za umma, ni chombo ambacho kimefanikiwa kuziweka pamoja pande mbili husika.

 

 

Habari Kubwa