Kakunda kusaka wanaoiga nembo

30May 2019
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Kakunda kusaka wanaoiga nembo

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, amekitaka kiwanda cha kuunganisha magari cha Rajinder kuwasilisha malalamiko ya baadhi ya watu kuiga teknolojia yao kwa maandishi kwa Tume ya Ushindani nchini (FCC).

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda

 

Alisema waigaji hao wanaodaiwa kughushi na kutumia nembo ya Rajender,  taarifa zao zikifikishwa kwa maandishi watashughulikiwa kwa wakati.

Aliyasema hayo jana wakati alipotembelea kiwanda hicho na kuwataka waandike barua rasmi  ili serikali iweze kushughulikia malalamiko hayo na hatua kali za kisheria zichukuliwe.

“Naiagiza tume ya usimamizi kuhakikisha inafika katika kiwanda cha Rajender na kushughulikia malalamiko hayo, ili kutokomeza na kudhibiti watu wasio waaminifu wanaotumia nembo ya Rajinder,” alisema na kuongeza kuwa

“Hatutamvumilia mtu yeyote atakayemsababishia mwekezaji hasara ya  kufunga kiwanda chake kwa ajili ya watu ambao si waaminifu wanaonakili na kukopi nembo ya mtu anayelipa staiki zote za serikali…”alisema.

Aliahidi kuwa serikali itamchukulia hatua kali za kisheria ili kutokomeza tabia hiyo.

Aidha, Waziri Kakunda alikitaka kiwanda hicho kusimamia usalama wa watu kazini ili kuepuka mamlaka zilizopo kuwapa adhabu.

“Pamoja na utendaji wenu mzuri unaofanyika naomba mzingatie zoezi la usalama kazini kwa wafanyakazi na utunzaji wa mazingira ikiwa ni hatua mojawapo ya ufanisi,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Manmohan Bhamva, alisema kinakabiliwa na changamoto kubwa ya watu kuigiza anachofanya huku akiiomba serikali kuangalia namna ya kutokomeza changamoto hiyo ili aweze kupanua kiwanda chake katika maeneo mbalimbali ndani na  nje ya nchi.

Alisema kwa sasa ametoa ajira kwa vijana waliomaliza mafunzo katika Vyuo vya  Ufundi (Veta) zaidi ya 200, lakini ana uwezo wa kuajiri zaidi.

Alisema mafanikio yataonekana iwapo  changamoto zake zitafanyiwa kazi kwa wakati.

“Leo ni kwa mara ya kwanza amekuja kiongozi mkuu katika kiwanda chetu. Sisi tunaona kama ni mafanikio makubwa na hii ni kutokana na ushirikiano mkubwa tunaoupata katika serikali kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa. Tutaendeleza kuzalisha kwa wingi na kulipa stahiki zote za serikali.

Kijana mkata vyuma, Samson Erick, akizungumzia mafanikio alisema mbali na kupata ajira amepata mafunzo maalumu ya namna ya kukata vyuma kwa kutumia kompyuta.

Habari Kubwa