Kamati kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji

15Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Kilwa
Nipashe
Kamati kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amewataka viongozi wa serikali kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji, kata na wilaya kuunda kamati za maridhiano kwa ajili ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo na kuleta madhara kwa jamii.

Ulega alitoa agizo hilo kwenye ziara aliyoifanya Kijiji cha Nakiu, wilayani Kilwa, mkoani Lindi Septemba 13, 2021 baada ya kupokea kero zilizohusu migogoro mingi iliyoanza kujitokeza katika wilaya hiyo inayowahusisha wakulima na wafugaji.

Katika mkutano huo wananchi wa kijiji hicho walililalamikia Jeshi la Polisi kutochukua hatua za haraka wanapopelekewa taarifa za wafugaji wanaolisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.

Walisema wafugaji wanaofanya vitendo hivyo wengi ni wahamiaji katika maeneo hayo na wanasababisha matatizo makubwa ikiwamo kuharibiwa kwa mazao yao na wanapotaka kulinda mazao yao wanaishia kupata kipigo.

Kufuatia malalamiko hayo, Waziri Ulega alitoa maelekezo kwa watendaji wa serikali kuanzia ngazi za chini kuanzisha kamati za usuluhishi ili ziwe zinashughulika na migogoro hiyo mapema kabla haijakuwa mikubwa na kuleta madhara.

Aliongeza pia kwa kulitaka Jeshi la Polisi wilayani humo kuhakikisha wanatenda haki kwa kila mtu na kwa usawa ili kuondoa lawama zinazowakabili za kuonekana wanawapendelea wafugaji kuliko wakulima.

Vilevile, aliwaelekeza watendaji wilayani humo kuwa katika kamati watakazoziunda waandae mpango mzuri wa kuweka njia kwa ajili ya kupitishia mifugo ili isiwe inapita katika mashamba ya wakulima.

Waziri Ulega pia kukemea vitendo vya kujichukulia sheria mkononi vinavyofanywa na wakulima pamoja na wafugaji akisema kuwa kufanya hivyo ni kosa na ni miongoni mwa vitendo vinavyochangia uvunjifu wa amani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa, katika kuhakikisha maelekezo hayo ya Naibu Waziri yanafanyiwa kazi kwa haraka aliwaagiza watendaji wake kuhakikisha kamati hizo zinaundwa ndani ya wiki moja.

Kuhusu suala la kuweka njia za mifugo, Kawawa alitoa mwezi mmoja kwa wataalamu wa mifugo kwa kushirikiana na wafugaji na wakulima kuhakikisha njia hizo zinawekwa ili kupunguza usumbufu wa mifugo katika mashamba ya wakulima.

Mkuu wa Wilaya pia aliwataka wafugaji kuchimba mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo na kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza migogoro ya mara kwa mara na wakulima.

Kabla ya ziara hiyo ya Waziri Ulega wilayani humo, siku chache zilizopita wafugaji waliuawa kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Nanjilinji.

Habari Kubwa