Kampeni yawavuta wakulima wa korosho

24Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Lindi
Nipashe
Kampeni yawavuta wakulima wa korosho

CHANGAMOTO ya huduma za kifedha iliyokuwa ikiwakabili wakulima wa korosho mikoa ya Mtwara na Lindi ikiwamo kutopata mikopo kwa wakati na makato ya fedha zao wanapofanya miamala ya kibenki, imetajwa kuwa miongoni mwa sababu kubwa za kuvutiwa zaidi na kampeni ya kuwahamasisha kuongeza uzalishaji.

Kampeni hiyo ambayo wanaeleza kuwa imewahamasisha ni ya ‘Vuna zaidi na NBC Shambani' inayoendeshwa na benki ya NBC mahususi kwa mikoa hiyo.

Wakizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo mkoani Lindi jana na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa zao hilo wakiwamo viongozi wa kiserikali, viongozi vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika, wakulima hao walisema ujio wa kampeni hiyo umewahamasisha zaidi kujiunga na huduma ya NBC Shambani ili kujikwamua kutoka kwenye changamoto hizo zilizotajwa kukwamisha jitihada zao za kujikwamua na umaskini kupitia kilimo cha zao hilo.

“Pamoja na uwapo wa zawadi mbalimbali kwenye kampeni hii kama baiskeli, pikipiki, pampu za kupulizia dawa, maguta  pamoja na matrekta zaidi pia tumevutiwa sana akaunti husika kwa kuwa inajibu changamoto kadhaa zinazotukabili kwenye huduma za kifedha ikiwamo ucheleweshwaji wa mikopo na makato yaliyokithiri,’’ alisema Swalehe Juma, Mwenyekiti wa Nachunyu AMCOS mkoani Lindi.

Walisema changamoto ya ucheleweshwaji wa mikopo imekuwa ikisababisha wengi wao kupata fedha wakati usio sahihi kulingana na mahitaji yao ya kilimo, hivyo kujikuta wakitumia mikopo hiyo kwa shughuli zisizoendana na kilimo.

“Tunashukuru kuona kwamba NBC wameamua kubuni huduma mahususi kwa ajili yetu… tukiwa kama viongozi wa vyama vya msingi tumeipokea vema huduma hii na tumejipanga kuhakikisha kwamba inawafikia wanachama wetu wote kwenye maeneo yetu,’’ aliongeza.

Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa, alisema licha ya uwapo wa huduma ya NBC Shambani kwa zaidi ya mwaka sasa benki hiyo imebuni kampeni hiyo ili kuhakikisha kila mkulima wa korosho anafikiwa na huduma hiyo ili kwa pamoja waweze kufikia adhma ya kuleta mapinduzi ya kilimo kupitia zao hilo.

“Nii kampeni inayolenga kuhamasisha mapinduzi ya kilimo cha korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ndio sababu hata zawadi zinazotolewa kupitia kampeni hii ikiwemo pikipiki, pampu za kupulizia dawa na matrekta zinalenga kumsaidia mkulima aweze kustawisha kilimo chake,’’ alifafanua.

Akizungumza wakati akifungua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mratibu wa uwekezaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Gaudence Nyamwihura, pamoja na kuwasisitiza wakulima hao na AMCOS kuchangamkia kampeni hiyo, pia aliwasisitiza kubainisha vipaumbele vyao wanapoamua kukopa kwenye taasisi za kifedha ili matumizi ya mikopo hiyo iwe na tija zaidi kwao.

Uzinduzi wa kampeni hiyo ulienda sambamba na uzinduzi wa huduma ya bima ya afya kwa wakulima wa zao hilo inayotolewa na benki hiyo kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja utoaji wa msaada wa pikipiki na baiskeli zilizotolewa na benki hiyo kwa AMCOS za mkoa huo kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kiutendaji.

 
 

Habari Kubwa