Kampuni iliyopigwa ‘stop’ yapewa tena

02Nov 2017
Marco Maduhu
Nipashe
Kampuni iliyopigwa ‘stop’ yapewa tena

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, limesikitishwa na kitendo cha utawala wa halmashauri hiyo kuipatia kazi kampuni ya ujenzi ya Ikonda kujenga chumba cha upasuaji katika kituo cha afya Kambarage wakati ilishapigwa marufuku kufanya kazi za halmashauri. 

Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Agnes Machiya.

Kampuni hiyo imekuwa ikituhumiwa mara kwa mara na madiwani hao kufanya kazi chini ya kiwango na kuingizia serikali hasara ya kufanya marekebisho ya muda mrefu kwenye miradi hiyo.

Hayo yaliibuliwa juzi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo wakati wakijadili taarifa ya Mkurugenzi na kubainika maazimio yao yamekiukwa.

Mmoja wa madiwani hao, Emmanuel Ntobi, kutoka Kata ya Ngokolo, alimtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kueleza sababu ya kampuni hiyo kupewa kazi nyingine wakati madiwani waliazimia isipewe kutokana na kutekeleza miradi chini ya kiwango.

“Nimesoma katika kablasha hapa naona kwenye ujengaji wa chumba cha upasuaji kwenye kituo cha afya Kambarage, tenda hiyo imepewa tena kampuni ya Ikonda, ambayo hapo awali tuliadhimia isipewe kazi tena hapa kuna nini kinachoendelea,” alihoji Ntobi.

Akitoa majibu hayo Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Geofrey Mwangulumbi, alisema hajawahi kuona maazimio hayo kwa kuwa alikuwa bado mgeni na hakuambiwa kama kampuni hiyo imeshapigwa marufuku.

Alisema hata hivyo, kampuni hiyo imeshaanza ujenzi wa chumba hicho, itakuwa vigumu kuizuia na kuahidi kumkabidhi mhandisi kuisimamia kazi hiyo hatua kwa hatua hadi ujenzi utakapokamilika.

Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Agnes Machiya, aliitaka ofisi hiyo kuzingatia maazimio yanayotolewa na madiwani hao, ili kuondoa msuguano kwa kuwa wao ndio wasimamizi wakuu wa miradi ya halmashauri hiyo.

Habari Kubwa