Kampuni ya kitalii yapiga 'jeki' vyumba vya madarasa

16Jan 2019
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Kampuni ya kitalii yapiga 'jeki' vyumba vya madarasa

KAMPUNI ya utalii ya Tanzania B James Safari, imejenga madarasa mawili katika Shule ya Msingi ya Oloitushula, iliyopo kata ya Musa, Halmashauri ya Arusha Vijijini, wilayani Arumeru kwa lengo la kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kampuni hiyo, wakati wa kukabidhi madarasa hayo, Weptak Kapaliswa, alisema kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma za kijamii na za kimaendeleo kwenye maeneo yote ambayo wanafanya shughuli zake za uwindaji.

Hata hivyo, Kapaliswa, hakutaja kiasi cha fedha ambacho kimetumika kujengea madarasa hayo.

Alisema sababu kubwa ya kujenga mradi huo wa madarasa ni kurudisha fadhila kwa jamii inayowazunguka kutokana na faida wanayoipata.

“Wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka kampuni yetu wanakuwa sehemu kubwa ya uhifadhi wa maliasili ya wanyamapori, hivyo, pamoja na sisi kupata neema ya kuvuna wanyama kwa kufuata sheria na taratibu za nchi, lakini ni lazima tuwe na kitu ambacho tutarudisha kwenye jamii ili na wao waweze kufaidia na uvunaji wa wananyama pori,” alisema.

Alisema kutoa mchango wa madarasa hayo kunaihamasisha jamii kuona thamani ya wanyamapori, uhifadhi na kutunza mazingira ambapo kwa kufanya hivyo inawasaidia kuwekeza zaidi katika kizazi kijacho hususani katika sekta ya elimu.

“Tunapoelimisha watoto tunawaelimisha kwa ajili ya kuwekeza katika maisha yao ya baadaye na nchi kwa ujumla kuwa na wasomi wengi waliosoma na kupata elimu bora,” alisema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Oloitushula, Ernest Lesikari, alisema katika kipindi cha mwaka 2018 wanafunzi walioandikishwa kijiunga na masomo kwa darasa la kwanza wamefaulu vizuri kwa asilimia 100.

Licha ya ufaulu huo, alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya madarasa, hivyo, amewataka wananchi kujitolea kwa michango na nguvu kazi ili kukabiliana na changamoto hiyo.

“Kwa kiasi kikubwa wananchi wamekuwa wakijitoa kwa kiwango kikubwa kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hizo ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma ufaulu kwa wanafunzi wetu.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dk. Wilson Mahera, alisema licha ya kukabidhiwa madarasa hayo, bado yamekosa madawati 48 hivyo wanahakikisha madawati hayo yanapatikana kwa wakati.

“Kabla ya bajeti ya mwaka huu halmashauri itahakikisha kwamba madawati yanapatikana kwa wakati ili wanafunzi waweze kusoma bila ya kikwazo chochote,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Elizabeth Mollel, alisema kuwa shule hiyo ina wanafunzi 525, na wanauhitaji wa vyumba vya madarasa 11 na kwa sasa wana upungufu wa madarasa manne.

Habari Kubwa