Kampuni ya simu itakayotoa taarifa za mteja kushughulikiwa

26Jan 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Kampuni ya simu itakayotoa taarifa za mteja kushughulikiwa

SERIKALI imesema itaichukulia hatua kali za kisheria kampuni yoyote ya simu itakayolalamikiwa kutoa taarifa za wateja.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile, alitoa kauli hiyo jana jijini hapa katika utiaji saini wa mikataba ya kupeleka mawasiliano vijijini awamu ya tano.

Alisema wizara hiyo itahakikisha inatunga sheria ya kuwalinda wateja wa simu za mkononi ili kuondoa tabia hiyo ya kutoa siri za wateja.

Alisema, kumekuwa na malalamiko kwamba kampuni za simu za mkononi zinatoa siri za wateja jambo alilosema sio sahihi kwa mujibu wa sheria ya kampuni hizo.

"Kumeanza kuzuka wimbi katika kampuni ya simu za mkononi kutoa siri za wateja, kitendo hiki ni kinyume cha sheria na kampuni itakayobainika watumishi wake kufanya hivyo, kampuni hiyo itachukuliwa hatua," alisema.

Alizitaka kampuni hizo kusoma sheria na kuielewa na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria huku akisema wapo watu mahsusi wanaoweza kupewa taarifa za mteja kwa mujibu wa sheria hiyo na siyo kila mtu.

Aliutaka Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), kupeleka mawasiliano katika maeneo yote nchini hasa ya mipakani ili nchi iondokane na kutumia mitandao ya nchi jirani.

Habari Kubwa