Kampuni yazindua teknolojia ya kisasa ya kutibu maji chumvi

25Nov 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kampuni yazindua teknolojia ya kisasa ya kutibu maji chumvi

KAMPUNI ya Tamgo ambayo inajishughulisha na utengenezaji wa mitambo ya kutibu maji, umeme wa nishati ya jua na majenereta imezinduliwa rasmi nchini.

Meneja Uendeshaji wa Tamgo, Henrik Nielsen.

Uzinduzi huo ulifanyika Dar es Salaam hivi karibuni huku Meneja Uendeshaji wa Tamgo, Henrik Nielsen, akibainisha kuwa lengo lao ni kutoa huduma bora za vifaa vya kisasa hapa vyenye ubora wa hali ya juu.

Nielsen alisema wamejipanga katika soko la ushindani la hapa nchini, lakini vifaa bora ndiyo nguzo yao kubwa ya kushinda soko.

Alisema wanajivunia uzoefu katika sekta ya utengenezaji mitambo ya kisasa na wamefanya hivyo katika nchi nyingi na kuamua kupanua biashara kwa kuwekeza Tanzania.

“Tunajua kuna ushindani mkubwa katika soko, lakini nguzo yetu kubwa ni kutoa huduma bora na za kisasa zaidi kama tulivyofanya katika nchi nyingi ambazo tumekuwa na biashara ya aina hii,” alisema Nielsen.

Meneja wa kampuni hiyo, Tarek Mostafa, alisema wanajivunia uwekezaji mkubwa wa teknolojia ya tiba za maji, majenereta na umeme wa nishati ya jua katika maeneo yote wanayofanya biashara duniani.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Maji ya kampuni hiyo, Damian Massenge, alisema wametengeneza mtambo wa kuchakata maji ya chumvi ujulikanao kwa jina Reverse Asmosis (RO) na kuwa maji matamu.

Massenge alisema teknolojia hiyo inapatikana kote nchini kwa muda mfupi na gharama nafuu akifafanua kwamba itasaidia kuondoa chumvi kwenye maji katika maeneo ambayo yana maji chumvi.

Alisema wamejifunza kutoka kwenye nchi za Ujerumani, Italia na Ufaransa na kufafanua kuwa upatikanaji wa maji ya chumvi ni rahisi hasa kipindi hiki cha ukame, hivyo wanapoyachakata na kuondoa chumvi itapunguza makali ya mgao kipindi hiki.

“Mitambo hiyo ya kisasa inazalishwa hapa hapa nchini na kuwarahisisha upatikanaji wake, hivyo kupunguza gharama tofauti na miaka ya nyuma ilikuwa lazima ikatengenezwe nje ya nchi na kuanza kuisafirisha ambapo gharama iliongezeka zaidi," alisema.