Kanuni za fedha kuzibana kampuni za mikopo umiza

25Feb 2021
Salome Kitomari
MTWARA
Nipashe
Kanuni za fedha kuzibana kampuni za mikopo umiza

KANUNI za huduma ndogo za fedha za mwaka 2018 za Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017, zimeweka utaratibu unaowataka wakopeshaji binafsi, kampuni za mikopo na wakopeshaji kidigitali kuweka wazi masharti ya mikopo na viwango vya riba visivyo vya asilimia.

Watoa huduma hao ambao kwenye sheria ametajwa kama daraja la pili, wanatakiwa wawe wamesajiliwa chini ya Sheria ya Kampuni au sheria nyingine huku wakopeshaji binafsi watatakiwa kusajili jina chini ya sheria ya usajili wa majina ya biashara.

Watoa huduma hao watatakiwa kuwa na jina la mtoa huduma ndogo za fedha kujumuisha maneno ya ‘Microfinance’ au “Finance’ au ‘Financial’ ‘Services’ au ‘Credit’ au ‘Microcredit’.

Aidha, wakopeshaji hao wanatakiwa kuwa na sera ya mikopo kwa mujibu wa sheria, kuhakiki uwezo wa mkopaji na kulipa mkopo, kuwapo mkataba wa mikopo ambayo itaeleza wazi masharti ya mkopo husika na urejeshaji wake ikiwamo viwango vya riba kwa kiasi (tarakimu) na siyo asilimia na vilifafanuliwe kwa mwezi na mwaka.

“Kanuni inataka kuweka bayana vigezo na masharti ya mkopo ikiwamo kiasi cha mkopo, kiasi cha riba kwa mwaka, ada zote, riba halisi kwa mwaka, mpango wa malipo, kiasi chote cha fedha kitakachokuwa kimelipwa hadi mkataba wa mikopo uishe,” alifafanua Meneja wa Huduma ndogo za fedha na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni wa BoT, Victor Tarimu.

Kanuni hizo zimetaja kuwa ni lazima wawe na mtaji wa chini kabisa wa Sh. milioni 20, kiwango cha chini cha mali zenye ukwasi asilimia 15 ya mali zote, kufanyiwa ukaguzi na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), uwasilishaji wa taarifa na BoT kuchukua umiliki wa mtoa huduma ndogo za fedha.

“Maombi yaambatane na ada ya Sh. 500,000 kwa kampuni na Sh. 300,000 kwa watu binafsi, pia benki itafanya tathmini ya uwezo wa kifedha, uzoefu, sifa na uadilifu wa wamiliki, wajumbe wa bodi na viongozi,” alisema.

Aidha, watu binafsi wenye mikopo inayozidi Sh. milioni 20 au wateja au wanachama zaidi ya 100 watapaswa kuunda kampuni na kukidhi/ kuzingatia matakwa ya kampuni.

Kanuni hiyo imebainisha kuwa iwapo vigezo na masharti yote yametimizwa BoT itatoa leseni katika kipindi cha siku 60 baada ya kupokea maombi yaliyokamilika.

Pia ni lazima kuwe na Bodi ya Wakurugenzi au chombo cha usimamizi kwa kampuni, majukumu ya bodi na uongozi, biashara inayoruhusiwa na isiyoruhusiwa, matumizi ya dhamana ya fedha taslimu au amana ya kulazimishwa.

Mengine ni utunzaji wa hesabu na nyaraka zingine, uandaaji na uwekaji wazi mahesabu, vigezo vya ukaguzi wa ndani na wa nje na kuwasilisha taarifa katika taasisi ya taarifa za mikopo.

Kanuni hizo zinataka kuwapo mfumo wa kushughulikia malalamiko ya wateja, utaratibu wa kukusanya madeni na utoaji elimu kwa mlaji.

Habari Kubwa