Kanyasu atoa neno hoteli kufunguliwa

03Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kanyasu atoa neno hoteli kufunguliwa

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, amepongeza uamuzi wa Hoteli ya Serena kufunguliwa tangu ilipofungwa kwa ajili ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona.

Alitoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam wakati akishiriki hafla ya kufungua hoteli ya Serena ambayo imekuwa ni muhimu katika kuwahudumia watalii wengi wanaotoka na kuingia kutoka nchi za nje kabla na baada ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Alisema uamuzi wa kufungua hoteli hiyo unatoa ujumbe mzito duniani kuwa Tanzania ipo salama na ipo tayari kwa ajili ya kuwapokea watalii.

Alisema kurudi kwa biashara hiyo kunarudisha uhakika wa maisha ya watu takribani 450,000 ambao wameajiriwa moja kwa moja katika sekta ya utalii.

Alisema ugonjwa wa corona uliiathiri jamii katika nyanja za kiuchumi na kijamii baada ya watu wengi kupoteza ajira na wengine kuachishwa kazi.

Alisema uamuzi wa kuifungua Hoteli ya Serena unaleta mwanga wa matumaini kwa Watanzania wanaoitegemea sekta ya utalii katika kuendesha maisha yao.

"Ninawashukuru Hoteli ya Serena kwa kupeleka ujumbe kwa wawekezaji wetu wote ambao wanaogopa na kufunga biashara zao kwa ajili ya ugonjwa huo.

Kanyasu alitoa wito kwa jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona na kuwa ugonjwa huo bado upo, lakini hauwezi kukimbiwa, hivyo ni lazima kujifunza kuishi nao.

"Tunamshukuru sana Rais John  Magufuli kwa kufanya maamuzi ya kufungua anga, ambapo tunaamini biashara ya utalii na biashara ya anga zinategemeana kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Alisema uamuzi huo umeifanya biashara ya utalii kurejea kwa kuwa tayari ndege za mashirika ya ndege ya Ethiopia, Emirates, KLM na Quatar zimeanza kuja nchini.

Naye, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Goldwin Mollel, aliwataka wadau wa sekta ya utalii kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa na wizara yake ili kuhakikisha usalama wa wageni na wenyeji wanaowahudumia watalii.

Akizungumzia uamuzi wa kuifungua hoteli hiyo, alisema inatuma ujumbe kwa wawekezaji wengine kuwa Tanzania ipo salama  na Watanzania wapo tayari kwenda nchi za nje kwa ajili ya kutafuta shughuli za biashara.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo, alisema tangu anga lilipofunguliwa kumeonyesha dalili njema ya ujio wa idadi kubwa ya watalii.

"Kuna matumaini makubwa ya kupata watalii wengi zaidi kwa mfano siku ya jana ndege ya Shirika la KLM ilitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ( KIA) ikiwa na abiria 200 kati ya hao 45 ni watalii waliokuja nchini kwa ajili ya kutalii," alisema Jaji mstaafu Mihayo.

Habari Kubwa