Kariakoo ilivyo hatarini kupata maambukizi

25Mar 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Kariakoo ilivyo hatarini kupata maambukizi

AGIZO la serikali la kuwataka wafanyabiashara kuweka maji na vitakasa mikono kwenye maeneo ya biashara zao, baadhi ya wafanyabiashara eneo la Kariakoo wameonekana kupuuza agizo hilo ambalo lina lengo la kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Nipashe ilishuhudia baadhi ya maduka sokoni humo yanayotembelewa na mamia ya watu yakiwa hayana ndoo zenye majisafi yenye mabomba ya kuyatiririsha, sabuni za maji na vitakasa mikono.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao walisema hawajaweka vifaa hivyo kwa sababu vinauzwa ghali.

Hussein Mjema ni mfanyabiashara wa vyombo vya nyumbani anayeuza eneo la Soko Kuu Kariakoo ambaye alisema kuwa hawajaweka vifaa hivyo kwa sababu hawajaelimishwa.

“Jumamosi na Jumapili nimeambiwa na wenzangu kuwa magari ya manispaa yalipita kutoa elimu ya matumizi ya vitakasa mikono au sabuni za maji na maji yanayotiririka.

“Baada ya wenzangu kunielimisha ndiyo tupo kwenye harakati ya kutafuta fedha ili kununua vifaa hivyo kwa ajili ya kujikinga sisi na wateja wetu.”

Muuza urembo sokoni hapo, Elia Jackson alisema elimu ya corona ameipata, lakini changamoto inayowakabili wafanyabiashara wadogo ni gharama ya vifaa hivyo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini ndoo maalumu ya kunawia mikono inauzwa kati ya Sh. 10,000 hadi 20,000, sabuni za maji zinauzwa kati ya Sh. 3,500 hadi 4,500 sokoni hapo.

Jackson alijitetea kuwa bei ya vitakasa mikono ni kubwa ndiyo maana asilimia kubwa ya wafanyabiashara hawajaweka.

“Sisi wafanyabiashara wadogo tunashindwa kuweka kwa sababu ukitazama misingi yetu ni midogo,” alisema.

Gazeti hili liliutafuta uongozi wa Soko Kuu la Kariakoo na kufanikiwa kuzungumza Meneja wa soko Donald Sokoni, ambaye alisema utaratibu waliouweka ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara wanaozunguka soko hilo ili kila mmoja awajibike kuweka vifaa hivyo.

“Tangu serikali itoe maagizo kuhusu virusi vya corona na kutaka maeneo yenye mikusanyiko yote yachukue tahadhari ikiwa ni pamoja na kuweka vifaa vya kunawia mikono, uongozi wa soko umefanya hivyo.

“Kutokana na gharama ya vitakasa mikono kuwa juu, tulipata ushauri kutoka ofisi ya Mganga Mkuu Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ambao walituelekeza tuchukue kidonge viwili vya chlorine ambavyo tunavichanganya kwenye ndoo ya maji ya lita 20 na kupata mchanganyiko wa kitakasa mikono.”

Alisema kwa siku soko hilo limekuwa likitumia ndoo 15 zenye mchanganyiko huo zinazowekwa kwenye milango 12 ya kuingilia ambazo hutumika kuwanawisha watu wanaoingia na kutoka ndani ya soko hilo ikiwamo shimoni.

“Tunawashauri wafanyabiashara sokoni hapa ambao mpaka sasa hawajaweka vifaa vya kunawia kwenye maeneo yao wafanye hivyo ili kutoruhusu ugonjwa huu kusambaa zaidi,” alisema.

Alisema kama bei ya vitakasa mikono ni kubwa, wanaweza kutumia mchanganyiko huo wa kidonge cha chloride au sabuni ya kawaida ya maji.

Pia alitaja changamoto nyingine ni baadhi ya watu ambao hawana makazi kulala sokoni hapo ambao wengine huwa ni wagonjwa.

“Kumekuwa na changamoto hii, kwa mwaka jana pekee walikuwa kama wanne, watu wa aina hii tunawataka wachukue tahadhari kwa maana akipata mmoja maambukizi ni rahisi kuambukiza wengi.

“Wanalala hapa na wengine wanazidiwa wanakuja kuomba msaada ukimuuliza vipi anakwambia siwezi kutembea, tunaangalia hali yake ikoje tukiona imezidi sana tunatoa taraifa Polisi na baadaye anapelekwa hospitali, wengine unakuja unakuta wamekufa usiku.”

Habari Kubwa