Katazo mifuko plastiki laibua fursa

28May 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Katazo mifuko plastiki laibua fursa

WAJASIRIAMALI jijini Arusha wamepata mafunzo ya muda mfupi
ya utengenezaji mifuko mbadala ya karatasi kwa ajili ya vifungashio 
ili kukabiliana na upungufu wa mifuko utakaojitokeza, baada ya
serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.

Wakizungumza jana katika hafla ya kuhitimu mafunzo ya wiki mbili ya
kutengeneza vifungashio kwa kutumia karatasi, katika Chuo cha Ufundi
cha

Tanganyika Polytechnic, baadhi ya wahitimu hao waliishukuru
serikali kwa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kuwa 
imewawezesha kupata fursa ya kujifunza kuzalisha mifuko mbadala
itakayowawezesha kujiajiri na kuongeza kipato.

Wakizungumza  kwa niaba ya wenzao, Martha Mwakidebe, Rose
Chisala  na Neema Mgendi, waliipongeza serikali kwa hatua ya kuzuia
matumizi ya mifuko ya plastiki, kwa kuwa 
imewapa fursa ya kujifunza na kuanzisha viwanda vidogo, kwa ajili ya
kuzalisha mifuko mbadala ambayo imeanza kuwanufaisha.

"Hii fursa itatusaidia sisi wajasiriamali kujiajiri kwa kutumia ujuzi
tulioupata kutengeneza mifuko mbadala, ili kupiga vita matumizi ya
mifuko ya plastiki," alisema Chitala.

Naye Meneja wa Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) Mkoa wa Arusha, Nina Nchimbi, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo hayo, aliwataka wahitimu
kutumia fursa hiyo kuanzisha viwanda vidogo,  kwa ajili ya kuzalisha
vifungashio. Alisema kwa kufanya hivyo watakuwa wanaunga mkono sera ya serikali kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.

Alikipongeza chuo cha Tanganyika Polytechnic kwa ubunifu na
kuanzisha mafunzo ya ufundi stadi yatakayowasaidia kujengea uwezo wa
kufanyakazi za kuzalisha kupitia ujuzi walioupata.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Abdul Semvua, alisema mafunzo hayo ni ya tatu
kuhitimu tangu waanzishe programu hiyo ambayo imelenga kuunga mkono
katazo la serikali kuhusu uzalishaji wa mifuko ya plastiki kwa kutoa
elimu ya ujuzi kwa wajasiriamali kuweza kutengeneza mifuko ya
karatasi."Tumekuwa na mafanikio makubwa tangu tuanzishe programu ya kutoa ujuzi kwa wajasiriamali kutengeneza mifuko ya karatasi na wengi
waliohitimu kwa sasa wanatengeneza vifungashio na wameanza kuonja
mafanikio," alisema Semvua.

Awali mbunifu wa mitaala katika chuo hicho, Dk. Richard Masika, alisema
nia ya chuo ni kujenga uwezo wa ujuzi kwa
wajasiriamali ili wawe na uthubutu wa kuanzisha viwanda vidogo na
kuondoa dhana iliyojengeka kwamba wenye uwezo wa kuanzisha viwanda ni
wageni kutoka nje ya nchi.

Alisema mbali na chuo hicho kutoa mafunzo ya ujasiriamali kinatoa
mafunzo ya ufundi wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), umeme wa jua na umeme wa nyumbani.

Habari Kubwa