Kaya 1,050 kunufaika na mazao viungo biashara

08Dec 2021
Rahma Suleiman
Pemba
Nipashe
Kaya 1,050 kunufaika na mazao viungo biashara

KAYA 1,050 nchini zinatarajiwa kufaidika na mradi wa kilimo hai cha mazao ya biashara ya viungo kupitia mradi wa Agri-Connect unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa Kongamano la kilimo hicho Chakechake, kisiwani Pemba, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Soud Nahoda Hassan, alisema ushirikiano wa taasisi za kilimo hicho kwa Zanzibar na Tanzania Bara utakuza maendeleo ya Tanzania.

Soud alisema Zanzibar lazima iendane na mchakato wa kuendeleza kilimo hai ili kutoa tija kwa wazalishaji na kuleta ustawi kwa wananchi na serikali kwa ujumla.

Alisema kilimo hai ni moja ya mambo ambayo yatasaidia kuingia katika sekta ya utalii kwa vile itakuza uingiaji wa wageni kufika nchini kuangalia na kununua bidhaa hiyo baada ya kujionea uzalishaji wa viungo hivyo.

Waziri Soud  alisema Tanzania ina aina 30 ya viungo hao vikiwamo karafuu, pilipili manga, tangawizi, vanila, pilipili kichaa, mdalasini, iliki na  mchaichai  ambavyo vinatumika kwa chakula na dawa.

“Kihistoria uzalishaji wa viungo kwa Tanzania uko vizuri hasa vile vinavyotoka Pemba, hivyo naomba ushirikiano baina ya taasisi hizi uendelee kwa kuleta faida kwa wazalishaji na serikali kwa ujumla,” alisema Soud.

Alisema mwaka 2015  Zanzibar ilikuwa ikizalisha tani 8,609 na tani 396 (asilimia 4.29) ilitumika kwa usafirishaii , lakini mwaka 2019 usafirishaji uliporomoka  licha ya kuongezeka kwa uzalishaji kwa tani 38,987 kwa mwaka.

Waziri alisema karafuu ni zao pekee ambalo lilikuwa likichukua zaidi ya asilimia 90 katika kusafirisha  kwenye soko la viungo duniani ingawa Tanzania ina mpango wa kuongeza usafirishaji wa viungo katika miaka 10 hadi 15 ijayo.

Akitoa maelezo ya mradi huo kwa wafadhili kutoka EU, Colin Scott alisema mpango huo unaofadhiliwa na jumuiya hiyo utaboresha maisha ya wakulima wadogo  katika Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania na Zanzibar.

Alisema kuwa utachangia ukuaji wa uchumi, maendeleo  na uwekezaji katika sekta binafsi, utengenezaji wa ajira na kuboreshwa kwa usalama wa chakula na lishe.

Hata hivyo, alisema utasaidia uboreshaji wa sera zinazojenga mazingira wezeshi na uwekezaji zaidi wa sekta binafsi, kuendeleza minyororo ya thamani kwa kuboresha uzalishaji, usindikaji na uuzaji.

 
 
 
 
 

Habari Kubwa