Kazi SGR pongezi nyingi kwa serikali

06Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kazi SGR pongezi nyingi kwa serikali

MOJA ya mambo ya kufurahisha ambayo ningependa Watanzania wengi wayashuhudie ni ujenzi wa reli ya kisasa au standard gauge railways (SGR), unaoendelea sasa.

Mataluma ya Reli yakiwa yameweka kwa ajili ya kutandikwa juu hili kujenga mradi wa SGR kwa upande wa Shirika la Reli nchini(TRC).

Kazi hiyo ya kujenga mtandao mpya wa reli ni kubwa , ikifanyika mchana na usiku  tena ikipita katikati ya mabonde, milima, tambarare na mito inafanyika kwa awamu.

Hivyo safari ya kuizuru reli hii nayo ni kwa awamu inaanzia Dar es Salaam kwenye stesheni ya Shauri Moyo kuelekea Morogoro hadi Dodoma, makao makuu ya serikali.

Nikiwa mmoja wa  wanahabari waliokuwa  katika ziara iliyoandaliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), nilikuwa na kiu ya kujifunza kinachoendelea kwenye ujenzi wa SGR na  tuliambatana na wabunge wa Kundi la Maendeleo Endelevu waliokuwa na lengo la kuufuatilia ili kuufahamu utekelezaji wa mradi huo, tunaanza safari.

Niseme  hivi  ukweli, nilichokishuhudia na nilichokuwa nikikisikia ni vitu viwili tofauti. Awali nilifahamu kuwa serikali imetenga zaidi ya Sh. trilioni 7.1 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa ambayo treni zake zitatumia umeme na zitakwenda kwa kasi tofauti na hizi za sasa. Jambo litakalorahisha usafiri lakini pia kukuza uchumi wa nchi na watu binafsi.

Sikuwa na haja ya kufahamu zaidi nini kinaendelea kwenye utekelezaji wa mradi huo lakini nilipopata fursa ya kutembelea nilijifunza mengi ambayo napenda kuyaelezea kwa wasomaji wetu.

Kwanza ni uchapaji kazi vijana wanajituma  wanapiga kazi, vyuma vikigongwa gongwa, watu wanaovyofanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano wa hali ya juu hatua kwa hatua.

Pia utaona magari yaliyobeba vifaa mbalimbali yakiwajibika utaelewa nini ninachokisema lakini pia vijana  wa Tanzania na  wageni wanavyoshirikiana kufanya kazi kwa bidii ama kweli utajua watu wapo kazini.

Ukianzia Shaurimoyo kuna  ujenzi wa daraja la juu la zaidi ya kilomita 2.5 litakalobadilisha pia mwonekano wa  Dar es Salaam likiendelea kujengwa kwa kasi, utaamini pia kazi inayofanyika si utani.

Akitoka Shaurimoyo unatua  stesheni ya  Pugu , hapo tuliaambaa na  barabara ya mkandarasi  Yepi Merkezi anayejenga reli hiyo kuelekea Soga, njiani tulijionea namna miamba ilivyopasuliwa, milima ilivyochongwa  na tuta la reli kutandikwa kwa ustadi,  hapo utajiambia waliopewa jukumu hilo wanalimudu.

Ukifika Soga ndipo ilipo kambi ya ujenzi wa reli hiyo unakutana na kiwanda cha mataruma yanajengwa kwa vyuma na zege. Hapo utafurahi zaidi ukaona reli iliyotandazwa juu ya tuta na ukitupa macho pembeni hayatataka kuondoka kwenye maeneo zinakopandwa nyasi za kisasa  kudhibiti uharibifu wa mazingira, hakika  ni kazi zilizotukuka.

Ukiondoka Soga, unafika Ruvu hapo unakutana na daraja kubwa lenye urefu wa mita 11 na upana wa zaidi ya mita sita  hapo ndipo Reli ya SGR inapopita juu ya  Barabara ya Morogoro , inayoanzia Dar es Salaam hadi Tunduma mkoani Mbeya. Katika eneo hilo treni itapita juu na magari yatakuwa chini. Ndiko darajani.

Maji ya mto Ruvu yako salama, kwani kinachoshangaza ni namna maji yalivyofinyangwa finyangwa kuweka njia ili kupitisha mitambo pasipo misukosuko wala kuharibu mazingira na taratibu za maumbile.

Hakika ukabihatika kuyashuhudia unaweza usiamini kama kazi hii inafanyika Tanzania tena na wataalam wengi wa ndani kuliko wa kigeni.

Kwa wale wanaopafahamu Kwala eneo lililoko jirani na mizani ya Vigwaza limejengwa sehemu  kubwa ambalo kwenye masuala ya reli huitwa ‘marshalling yard’ ndiko treni yenye urefu wa kilomita mbili huunganishwa na pia ni sehemu ya kupishania. Pembeni  kidogo kuna  bandari kavu itakayokuwa inapokea na kuhifadhi shehena mbalimbali .

Panapofuata ni  Ngerengere, hapo ni Morogoro kuna shughuli nyingine nyingi zinazoendelea za ujenzi wa reli ya kisasa na kutoka stesheni hiyo unaingia Morogoro mjini huko utashuhudia mitambo inavyofanya kazi kwa kasi.

Kazi inafanyika mchana na usiku na kila mahali unakutana na malori  yanayobeba vifusi na vifaa vingine vingi vya ujenzi wa SGR..

Kikubwa na cha kuridhisha nilipowauliza kama wanalipwa fedha zao kwa wakati kama ambavyo wanafanya kazi kubwa na nzuri kwa juhudi, walinihakikishia wanalipwa tena kama walivyokubaliana kabla ya kupata kazi.

Tukitoka Morogoro sasa kuelekea Dodoma kupitia Kilosa na Gulwe, kazi inayoendelea ni kuchonga milima ya Kilosa ili reli ipite katikati badala ya kuizunguka  kama ilivyokuwa reli ya awali iliyojengwa na Mjerumani.

Baada ya kutoka Kilosa mambo yalianza kubadilika kwani tunaingia Mpwapwa , Dodoma yaliko makao makuu ya nchi, huko utajionea namna vijana wanavyopiga kazi mchana na usiku kusafisha tuta la reli kuelekea Ihumwa  hakika serikali inahitaji pongezi za dhati.

Ukiulizia ajira zilizopatikana ni takribani Watanzania 5,900 ambao wanafanya kazi ujenzi wa mradi huu utakaodumu bila marekebisho kwa karne nzima zaidi ya miaka 100.

Mbali na hayo kuna madaraja ya kutosha yanajengwa, njia za juu,  za chini, vivuko, majengo ya stesheni na maeneo ya biashara katika stesheni zote ili wananchi wapate huduma muhimu wakati wakisubiri treni au baada ya kushuka kwenye SGR.

Pamoja na ujenzi huo kuna kutoa mafunzo kwa wakandarasi wazawa, madereva wa kuendesha  treni na wataalam wengine kama mafundi kuhusu ujenzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa wataalam wa kimataifa.

Mpango wa serikali ni kuhakikisha reli inaanza kufanya kazi mwaka 2020 na kwa niliyoyaona na kasi niliyoishuhudia haya inawezekana na Watanzania tunapaswa kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kuliletea taifa maendeleo.

WABUNGE

Wabunge hao ambao walikuwa na shauku ya kufahamu na kushuhudia yale waliyokuwa wakiyasikia au kuyaona kupitia vyombo vya habari, wanasema wamevutiwa na mambo mapya na mageni waliyoshuhudia.

Kubwa linalowashangaza ni kuona taruma moja linalotengenezwa kwenye kiwanda cha  Soga, likitumia kilo 118 (mifuko  miwili na ushee  ya sementi) kutoka viwanda vya ndani.

Pia wanaelezwa kuwa taruma hilo linalotumia saruji nyingi linaweza kuishi zaidi ya miaka 100 kabla ya kufanyiwa ukarabati.

 

Wanasema  wanashangazwa kuona nguzo moja ya daraja la juu ikiwa na uzito wa tani 60 na tayari nguzo 102 zinashajengwa pamoja na ubora wa miundombinu inayojengwa na wakandarasi wazawa.

Mbunge wa jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi, anasema kazi kubwa inayofanyika kwenye ujenzi huo wa reli inafurahisha tena inaridhisha. “Kazi ni nzuri tumeshuhudia mambo ambayo tulikuwa hatuyafahamu kuhusu mradi huu," anasema Shangazi.

WATAALAMU TRC

Meneja mradi huo, kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, Machibya Masanja, anawaeleza wabunge hao kuwa, utekelezaji wa mradi huo, upo katika sehemu tano, kuanzia Mei 2017 hadi Novemba 2019.

Anaeleza kuwa  baada ya kukamilika kutakuwa na vivutio katika njia zote kama nyumba za asili na mambo ya kitamaduni.

Masanja anasema sehemu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo ina urefu wa kilomita 1,219 bila kujumuisha njia za kupishana akianza na kipande kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye kilomita 300, itakayokuwa na kilometa 205 za njia kuu na kilometa 95 za kupishana.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli (TRC), Masanja Kadogosa, awamu ya pili ya ujenzi ni wa kuanzia Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma wenye urefu wa kilomita 422 ikiwamo kilomita 336 za njia kuu na 86 za kupishana.

Sehemu nyingine ya kipande cha kutoka Makutopora hadi Tabora  cha kilometa 376.5 yenye njia 294 wakati eneo la kupishana ni  kilometa 73.5.

 

 

 

 

Habari Kubwa