KCB yatamba kufanya vizuri sokoni

08Feb 2016
Cynthia Mwilolezi
Nipashe
KCB yatamba kufanya vizuri sokoni

BENKI ya Ushirika ya Mkoa wa Kilimanjaro (KCB), imepokea zaidi ya Sh. milioni 671, kutoka programu ya miundombinu ya masoko, uongezaji thamani na huduma za fedha vijijini (Mivarf), kwa ajili ya kuboresha shughuli za uendeshaji katika benki hiyo kati ya mwaka 2012 na 2015.

Waziri wa Fedha Dk. Philip Mipango

Ofisa Kiungo (Focal Person), katika benki hiyo, Joseph Kingazi alisema fedha hizo zimesaidia kuimarisha utendaji wa benki ya KCB na kuiwezesha kutoa huduma bora kwa wateja wake na kwamba Mivarf ilianza kutoa fedha mwaka 2011/2012.

Kingazi alisema fedha hizo pia zilielekezwa kuiwezesha KCB kupanua huduma zake, ili kuongeza idadi ya wateja wake na kuiwezesha benki kukuza hisa na amana.

Alisema benki hiyo inafanya kazi na vyama vya ushirika wa akiba na mikopo, vikundi pamoja na vyama vya ushirika vya msingi vinavyojihusisha na ukusanyaji wa zao la kahawa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo mkoani Kilimanjaro.

Aidha, alisema benki hiyo hivi sasa ina wateja wapatao 50,000 ambao wamefungua akaunti za elimu kwa ajili ya watoto wao inayojulikana kama Deposit ya mtoto ambayo amesema imesaidia zaidi kukuza akaunti katika benki hiyo kufikia zaidi ya Sh. milioni 257 mwaka 2011/2012.

Kutokana na hatua hiyo ya Mivarf, benki hiyo imefanikiwa kukuza amana zake kwamba imeongeza huduma ya kutoa mikopo kwa wateja katika kipindi hicho kutoka Sh. bilioni mbili (2012) hadi Sh. bilioni 4.4 (2015).

Alisema idadi ya wateja wenye amana katika benki hiyo KCB wamefikia zaidi ya 449,969 ambapo kabla ya Mivarf kutoa ruzuku hiyo idadi ya wateja walikuwa 100,000.

Aidha, benki imeweza kutoa mikopo kwa wateja moja kwa moja wapatao 29,100.

Habari Kubwa