KCMUCO kuboresha miundombinu kwa bil. 2/-

12Jan 2018
Mary Mosha
Nipashe
KCMUCO kuboresha miundombinu kwa bil. 2/-

CHUO cha Kikristo cha Tiba Kilimanjaro (KCMUCO) kinatarajia kutumia zaidi ya Sh. bilioni mbili, kuimarisha miundombinu ya ufundishaji, ili kutimiza vigezo vilivyowekwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).

Akitoa taarifa ya chuo hicho jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mkuu wa chuo hicho, Prof. Egbert Kessy, alisema moja ya upungufu uliojitokeza na kusababisha kufungiwa kudahili wanafunzi ni wataalamu wa kufundisha na ukosefu wa maabara.

Alisema baada ya kufungiwa walichukua hatua mbalimbali za kuimarisha miundombinu ya kufundishia na mwezi Machi, mwaka huu watakuwa wamekidhi vigezo vya TCU na kusubiri ukaguzi, ili kuruhusiwa kudahili wanafunzi katika mwaka wa masomo ujao.

“Tulifungiwa kudahili wanafunzi katika mwaka huu wa masomo sababu kubwa ilikuwa ni upungufu wa walimu katika fani mbalimbali, ikiwamo ya Anatomy ngazi ya profesa na maabara ya Anatomy, Physiology, Biochemistry, Microbiology na Pharmacology, lakini tumeanza kuchukua hatua za kuajiri walimu hao na kutangaza nafasi katika masomo muhimu ambayo yalionekana kuwa na upungufu wa walimu, na kujenga jengo la maabara ambalo litakamilika kabla ya mwezi Machi, mwaka huu,” alisema Prof. Kessy

Mkuu wa mkoa Mghwira alisema, chuo hicho kuzuiwa kudahili wanafunzi kwa mwaka huu, ni changamoto kubwa katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa madaktari nchini.

Mghwira alisema, juhudi za chuo hicho zinahitajika ili kuhakikisha wanakidhi vigezo vya TCU na kuruhusiwa kudahili wanafunzi katika mwaka wa masomo ujao.

Alifika chuoni hapo kuona kinavyojiendesha na kushughulikia changamoto zilizosababisha kizuiwe kudahili wanafunzi katika mwaka huu wa masomo.

Habari Kubwa