Kiama zana feki

15Jun 2018
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Kiama zana feki

NAIBU Waziri wa Viwanda, Baishara na Uwekezaji, Stella Manyanya, amezitaka mamlaka za serikali kuhakikisha zinachukua hatua kali dhidi ya watu wanaoingiza nchini pembejeo zisizo na ubora kwa kuwa zinasababisha hasara kubwa kwa wakulima.

NAIBU Waziri wa Viwanda, Baishara na Uwekezaji, Stella Manyanya.

Manyanya alitoa agizo hilo juzi jioni alipokuwa akizindua Kanuni za Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini za Mwaka 2018.

Alisema kanuni hizo pamoja na mambo mengine, zinataka zana zote za kilimo zinazoingizwa na kutengenezwa nchini zinakaguliwa na mamlaka husika kujiridhisha kuhusu ubora wake hazijawafikia walaji (wakulima).

"Sasa tunajenga viwanda na uwezeshaji wake. Sisi kama wizara, tumejipanga kufanya mambo tofauti na ilivyokuwa imezoeleka kwa sababu tunajua tunakotakiwa kwenda," Manyanya alisema.

"Tunahakikisha tunakuwa na kanuni zinazolinda teknolojia yetu ya ndani tukizingatia kuwa hali ya sasa kumekuwa na mwamko mkubwa wa wadau kuleta zana kutoka ndani na nje ya nchi.

"Kuna zana nyingine zinaweza zisiwe na viwango na zinakuwa na hasara kubwa kwa aliyenunua. Msambazaji pia anaweza kupata hasara zinapogundulika zina tatizo.

"Tunazo sheria zinazotulinda na zinatutaka kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zinakuwa na viwango bora. Sasa tuhakikishe tunakuwa na zana zinazostahili.

"Nategemea sasa tutahakikisha kila zana za kilimo zinazoingia nchini zinakuwa na ubora. Taratibu zifuatwe na kila mmoja anayehusika na udhibiti wa zana za kilimo."

Alisema kuwa kila zana ya kilimo itakayoingizwa nchini ni lazima ikaguliwe kuhakikisha Tanzania haiwi jalala la kutupia zana mbovu.

Manyanya alisema ukaguzi wa kina wa zana hizo unapaswa kufanyika ili Tanzania isiendelee kuwa mahali pa majaribio ya teknolojia za mataifa ya nje.

"Kila kifaa kupitia kanuni hizi, sasa kitapita kwenye mamlaka za uchunguzi. Bidhaa zote zikaguliwe kuona kama zinakidhi vigezo ili kuhakikisa Tanzania haiwi mahali pa majaribio ya teknolojia," alisema.