Kibano kodi kwa wachimba madini

20Nov 2019
Alphonce Kabilondo
Geita
Nipashe
Kibano kodi kwa wachimba madini

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko, amewataka wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini nchini vikundi, kampuni inayozalisha madini kulipa ushuru wa huduma ya uwajibikaji kwa jamii na kodi ya huduma.

Biteko alitoa kauli hiyo mkoani Geita wakati akiweka jiwe la msingi kwenye zahanati ya gereza la Wilaya ya Geita inayojengwa kwa ufadhili wa Halmashauri ya Mji wa Geita na Mgodi wa GGML kupitia fedha ya wajibikaji wa makampuni.

Biteko amesema kila mgodi unaomilikiwa na kikundi ,kampuni ambao unazalisha madini unatakiwa kulipa huduma ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na kodi ya huduma.

Waziri huyo alisema wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini wanatakiwa kutambua kuwa tozo hizo si kwa kampuni kubwa pekee kama GGML bali ni kwa mgodi yote yenye leseni za uchimbaji zinazozalisha madini hayo.

Biketo alisema lengo la serikali ni kuhakikisha mikoa iliyojaliwa kuwa na madini inasongambele kimaendeleo ukiwemo mkoa wa Geita.

“Wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini, kikundi ,makampuni , kila mgodi unaozalisha madini hakikisheni mnatoa kwenye halmashauri husika fedha ya uwajibikaji wa kampuni katika jamii pamoja na kodi ya huduma ya tozo hii siyo kwa kampuni kubwa pekee bali kila mmiliki wa leseni ya madini anaezalisha madini,” alisema Waziri Biteko.

Pia waziri huyo amewataka wawekezaji nchini wa sekta ya madini kampuni kuzingatia sheria ya( Local Courntent )kwa kuwapa kipaumbele wazawa katika ajira ,pamoja na biashara.

Awali Mkuu wa gereza la Geita, Mussa Mkisi, akisoma taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo kwa Waziri Biteko, alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwezi julai mwaka huu ambapo sh. milioni 108 zimetumika kwa hatua ya kwanza.

Mkisi alisema zahanati hiyo ikikamilika itatoa huduma ya ushauri wa kitalaam na vipimo kwa majeshi yote askari polisi ,magereza, wafungwa pamoja na wananchi wote wa Mji wa Geita.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Leonard Bugomola, alisema Halmasahuri ya Mji imejenga zahanati tatu kupitia fedha ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii kutoka Mgodi wa GGM ambazo zimekamilika kwa asilimia 100 zinasubiri kufunguliwa.

Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu, alisema Halmashauri ya Mji Geita inatarajia kufungua zahanati mpya tatu zitakazosaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita huku akilipongeza jeshi la magereza kwa ujenzi wa zahanati hiyo.

Kanyasu alisema kuwa mwaka 2015 Halmashauri ya Mji wa Geita ilikuwa ikikusanya Sh. bilioni 1.8 kwenye mapato yake ya ndani lakini mwaka 2017 baada ya sheria ya kurekebishwa makusanyo yameongezeka .

Habari Kubwa