Kicheko wadau mnada kutofungwa 

13Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kicheko wadau mnada kutofungwa 

SERIKALI imewatoa hofu wananchi na wafanyabiashara kuwa haina mpango wa kufunga mnada wa mifugo wa Kasesya ulioko mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Badala yake, serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imesema inakusudia kuimarisha zaidi minada yote ya mipakani ili kutoa huduma bora za mifugo na mazao  itakayowezesha kuongeza ukusanyaji mapato.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia Mifugo, Dk. Maria Mashingo, baada ya kutembelea Kiwanda cha Kusindika Nyama cha Sumbawanga Agricultural and Animal Feed (SAAFI) kilichoko mjini Sumbawanga na kupokea maombi ya mwekezaji huyo.

Dk. Mashingo alisema nia ya serikali ni kufungua minada mingi maeneo ya mipakani ili kurahisisha uuzaji wa mazao ya mifugo kwenda nje ya nchi na kuchochea ukuaji uchumi kwa wafugaji na serikali kwa ujumla.

Aidha, Dk. Mashingo alisema uamuzi wa kufungwa kwa mnada huo, unategemea maoni ya wadau wengi na si uamuzi wa wizara  peke yake huku akiutaka uongozi wa kiwanda hicho kuanza uzalishaji wa nyama na mazao mengine ya mifugo kiwandani hapo ili kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa SAAFI, Paul Mzindakaya, alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuchinja ng'ombe 300 na mbuzi 800 kwa siku na kubainisha kuwa wanatumia teknolojia ya kisasa na ndicho kiwanda kikubwa cha kisasa kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Alisema kiwanda hicho kina maabara ya kisasa kwa ajili ya uchunguzi na upimaji ubora wa nyama kiwandani kabla ya kusafirisha kwa walaji na kwamba kama mitambo ya kiwanda hicho itatunzwa vizuri, inaweza kudumu kwa miaka 40 ijayo.

 Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kwa sasa kiwanda  hicho ndicho kinachoongoza kwa kuzalisha nyama bora na bidhaa zake hapa nchini.

"Nyama zote na bidhaa nyingine zinazotokana na mifugo zinazozalishwa hapa kiwandani ni za asili.  Nyama  inayozalishwa hapa ndiyo ‘halal’ (inayokubalika kimataifa) kwa sababu tumezingatia kanuni zote wakati wa uwekaji mitambo," alisema.

Alisema SAAFI imewahi kuwa mshindi wa kwanza kitaifa kwa uzalishaji wa nyama bora katika mashindano ya nje ya nchi  na kwamba pia nchi imewahi kuwa mshindi wa pili kati ya nchi tano zilizokuwa zinashindanishwa.

“Hatuna tatizo la soko la nyama hapa nchini na nje ya nchi. Tuliwahi kupata soko Zambia ambako tulikuwa tukiuza nyama tani 25 kila wiki. Pia tuliwahi kupata soko katika nchi za Angola na Oman,” alisema. 

Habari Kubwa