Kicheko wanakijiji kupata umeme Rea

22May 2020
Na Mwandishi Wetu
Tabora
Nipashe
Kicheko wanakijiji kupata umeme Rea

WAKAZI wa Kijiji cha Loya wilayani Uyui mkoani Tabora, wameishukuru serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kuwaunganisha na kuwawashia umeme katika kijiji hicho waliokuwa wakiona kama ndoto.

Walieleza hayo baada ya Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, kuwasha umeme katika kijiji hicho na kukagua maendeleo ya usambazaji, juzi.

Walisema, miaka mingi wamekuwa wakipewa ahadi zisizotekelezeka na wakati mwingine wakikatishwa tamaa ya kupata umeme kwa kuwa kijiji hicho kiko umbali mrefu kutoka ilipo miundombinu ya umeme na jiografia isiyo rafiki kufika maeneo hayo.

“Huyu waziri ameandika historia hapa Loya, haijawahi kutokea kiongozi mkubwa ngazi ya waziri kufika katika kijiji chetu tangu kimeanzishwa, wengi wanakuja katika wilaya hii, lakini wanaishia huko mijini tu, vijijini hawafiki,” alisema mwanakijiji Josephat Wamalulu.

Dk. Kalemani kwa upande wake alisema baada ya kusikia malalamiko na kuona uhitaji mkubwa wa umeme kwa kijiji hicho ambacho hakijafikiwa na mradi wa kusambaza umeme (REA) kwa kipindi hiki, aliliagiza Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kupeleka umeme kwa gharama zao katika kijiji hicho.

Alisema kijiji cha Loya kina wakulima wengi wa mpunga, karanga na wafanyabiashara ambao wanahitaji huduma ya umeme katika kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Tanesco ilitenga zaidi ya Sh. bilioni tatu ili kuhakikisha umeme unafika katika kijiji hicho, ambacho kiko umbali mrefu kutoka ilipopita miundombinu ya umeme.

“Niliwaagiza Tanesco kuleta umeme hapa Loya, kama mlivyoona ina wakazi wengi wakulima na wafanyabiashara ambao wanahitaji umeme katika shughuli zao,” alisema.

Vile vile, Tanesco iliagizwa kuendelea kusambaza na kuwasha umeme kwa wakazi wa eneo hilo waliokwisha kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ndani ya siku saba baada ya kulipia.

Aliwataka wakazi wa Loya kutumia umeme huo kujiendeleza kiuchumi badala ya kuutumia kuwasha taa peke yake.

Mbunge wa Jimbo la Igalula, Musa Ntimizi, aliwataka wafanyabiashara katika kijiji hicho kutanua wigo wa kibiashara na wakulima wa mpunga kuongeza thamani ya mazao yao ili kupata faida zaidi.

Habari Kubwa