Kilimo mpunga chawainua vijana

26Oct 2020
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Kilimo mpunga chawainua vijana

WATAFITI wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamebaini kilimo biashara cha zao la mpunga kinacholimwa kwa wingi katika Bonde la Kilombero mkoani Morogoro, hivyo kuwainua kiuchumi vijana wa Wilaya ya Kilombero.

MPUNGA.

Prof. Ntengua Mdoe, alisema kupitia mradi wa Utafiti wa Sera za Kilimo Barani Afrika (APRA), wamebaini vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 ambao ni sawa na asilimia 35.5 ya watu ndio wenye kunufaika zaidi katika bonde hilo.

Alisema hayo wakati akiwasilisha utafiti wake kwa waandishi wa habari wa kwenye warsha iliyoandaliwa na APRA.

Alisema pamoja na kuonyesha ushiriki wa vijana kwenye kilimo hicho, lakini bado wanakabiliwa na vikwazo ikiwamo ukosefu wa mitaji na mashamba ya uhakika ya kuendeshea kilimo hicho wengi wao wamekuwa wakikodi.

“Watafiti tumebaini kuwa sio kweli kwamba vijana hawashiriki kwenye shughuli za kilimo, bali wanashiriki vizuri kwenye kilimo cha mpunga na mpaka kwenye mnyororo wa thamani wa zao hilo katika maeneo mbalimbali,” alisema Prof. Mdoe.

Alieleza kwenye utafiti huo umebaini vijana hao wamekuwa wakijipatia kipato kikubwa kinachotokana na kuwekeza katika kilimo hicho na kufanyia shughuli za maendeleo kuliko nguvu inayowekezwa na vijana wanaofanya kazi zingine nchini.

“Kwenye utafiti wetu tumeshuhudia kuwa nyumba nyingi zinazoongozwa na vijana zina uhakika mkubwa wa chakula kuliko kaya ambazo zinaongozwa na wazee na watu wenye umri mkubwa, na hii ni kutokana na mafanikio makubwa wanayoyapata kutoka kwenye kilimo,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika mapendekezo ya utafiti huo wamezitaka halmashauri za wilaya na serikali kutenga ardhi ya kilimo kwa ajili ya vijana kama ambavyo imeelekezwa kwenye Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 ili kuwaondolea changamoto na kusaidia Taifa kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga.

Mapendekezo mengine ni kuwapo kwa njia sahihi ya kuwasaidia vijana hao mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana pamoja na fedha zinazotolewa na halmashauri ya asilimia 10 kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambapo vijana wametengewa asilimia nne.

Naye Mkuu wa Mradi wa Utafiti wa Sera za Kilimo Barani Afrika upande wa Tanzania, Prof. Aida Isinika, alisema vijana wengi wanapenda kushiriki kwenye kilimo chenye tija na soko zaidi kama vile kilimo cha mpunga, vitunguu, nyanya na mazao mengine.

Habari Kubwa